Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laternano, hivi karibuni kimezindua rasmi Mwaka wa Masomo
2013- 2014, chini ya uongozi wa Baba Mtakatifu Francisko, tukio ambalo limezinduliwa
na Kardinali Augustino Vallini, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma na Mkuu wa Chuo Kikuu
cha Kipapa cha Laterano.
Kardinali Vallini ameitaka Jumuiya ya wanafunzi wa
Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano, kufanya tafakari ya kina kuhusu matukio makuu
ya historia ya Kanisa, yaliyoshuhudia kwa unyenyekevu mkuu Baba Mtakatifu Benedikto
XVI aking’atuka kutoka madarakani kwa hiyari yake mwenyewe kwa ajili ya ustawi na
maendeleo ya Kanisa la Kristo.
Kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu Francisko, limekuwa
ni tukio jingine ambalo limewaacha walimwengu wakiwa wameshika tama kwa mshangao mkubwa.
Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI ameacha urithi mkubwa ambao pamoja na mambo mengine
ni changamoto ya kuutafuta ukweli. Hii ni dhamana nyeti kwa wasomi ndani na nje ya
Kanisa; ni utume unaopaswa kuendelezwa na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya
juu zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa.
Wasomi wautafute ukweli katika
medani mbali mbali za maisha na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuanzisha mchakato wa
kutafuta ili waweze kupata ukweli katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ili kufanikisha
lengo hili kuna haja ya kuwa na uhuru wa ndani, unaoiwezesha akili kusafisha yale
yasiokuwa na umuhimu katika maisha, kwa kuzingatia ukweli.
Baba Mtakatifu
Francisko mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa, aliwataka Makardinali na
Taifa la Mungu katika ujumla wake kuzingatia mambo makuu matatu: kutembea, kujenga
na kuungama imani kwa Kristo na Kanisa lake. Hii ni dira makini kwa Jumuiya ya Wasomi
kuizingatia.
Chuo Kikuu hakina budi kuendeleza mchakato kwa njia ya tafiti
kwa ajili ya mafao ya wengi; kipindi cha masomo, iwe ni fursa kwa wanafunzi kujengeka:
kiakili, kiutu na kimaadili, kwa kujenga na kukuza kiu ya kutafuta ukweli na kumuungama
Yesu Kristo Mkombozi wa dunia kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji.
Askofu
mkuu Enrico Covolo, Makamu mkuu wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Laterano anasema kwamba,
mwaka wa masomo 2013- 2014 unajikita zaidi katika shughuli za kichungaji kwa wanafunzi
wa Chuo kikuu cha Laterano. Lengo ni kujenga na kuimarisha Jumuiya ya Chuo Kikuu cha
Kipapa cha Laterano. Utekelezaji wa mikakati hii unajikita katika masomo, hapo Majaalim
wanapaswa kutekeleza utume wao kwa kusukumwa na mfano wa Kristo mchungaji mwema, ili
kuwasaidia wanafunzi kuweka uwiano safi kati ya akili na imani.
Kardinali Zen
Ze Kiun, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong, China akitoa mhadhara wake
kwa kuzingatia mchango wa Kardinali Henry Newman, anaasema, Jaalim anapaswa kuwa ni
mlezi na mchungaji anayetekeleza wajibu na utume wake kwa niaba ya Mama Kanisa. Wanapaswa
kuwafahamu na kuwasaidia wanafunzi wao kufikia ukomavu wa kiakili na kiimani, tayari
kushiriki katika kuchangia elimu waliyoipata kwa ajili ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu.
Wanawajibika kushirikisha hekima waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa jirani zao.
Majaalim wajitahidi kuwa kati na kwa ajili ya wanafunzi wao kama alivyojitahidi
Mtakatifu Don Bosco kwa vijana wake; kama alivyofanya Yesu miongoni mwa wafuasi wake.
Jumuiya ya Chuo kikuu ni sehemu ya mchakato kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa
kwa siku za usoni.
Kardinali Zen Ze Kiun anasema, uhuru wa kidini nchini China
unazongwa mno kiasi kwamba, Kanisa Katoliki haliwezi kutekeleza vyema wajibu na dhamana
yake katika majiundo ya wanafunzi. Sheria mpya iliyotungwa hivi karibuni, imeliondolea
Kanisa uwezo wa kuongoza shule zake 300 na badala yake imeundwa Tume itakayowajibika
moja kwa moja kwa Serikali. Chuo Kikuu cha Kipapa, kinatarajia tarehe 21 Novemba 2013
kutembelewa na Rais Giorgio Napolitano wa Italia.