Wanawake wana mchango mkubwa katika kukuza na kudumisha misingi ya amani, ikiwa kama
watawezeshwa!
Mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni uliohitimishwa hivi karibuni
mjini Busan, Korea ya Kusini imekuwa ni fursa ya kuweza kuchambua maana na umuhimu
wa amani katika kukuza na kumwendeleza mwanadamu: kiroho na kimwili. Wajumbe wamechambua
maana ya amani ndani na nje ya Kanisa, wakiongozwa na kauli mbiu “Mungu wa uhai, tuongoze
katika haki na amani”.
Baadhi ya
wajumbe kutoka Afrika wamebainisha kwamba, kwa kuwawezesha wanawake katika masuala
ya misingi ya haki na amani, waliweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mchakato
wa haki, amani na upatanisho nchini Liberia, iliyokuwa imemezwa na machafuko ya vita
ya wenywe kwa wenyewe iliyosababisha majanga na madhara makubwa kwa wanachi wa Liberia.
Wajumbe wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wameyataka Makanisa kuhakikisha
kwamba, yanashiriki kikamilifu katika kuzuia, kuponya na kujenga misingi ya haki na
amani na kamwe yasiwe ni watazamaji wakati wa migogoro, machafuko na vita katika Jamii
husika. Katika mchakato kama huu, Makanisa yaoneshe dhamana yake kwa kusimama kidete
kutetea misingi ya haki na amani, hata kama yatasigana na Serikali zilizoko madarakani,
kwani kuunga mkono vitendo vya uvunjaji wa haki msingi za binadamu zinazofanywa wakati
mwingine na Serikali husika ni kuwavunja moyo wananchi.
Makanisa yajihusishe
katika mchakato wa haki, amani na upatanisho, ili Jamii ziweze kupata amani ya kweli
inayopata chimbuko lake katika maisha ya mwanadamu, amani ambayo ni dumifu! Wajumbe
wamesema kunako Mwaka 1953 Korea ya Kusini na Kaskazini zilitiliana sahihi mkataba
wa amani, lakini tangu wakati huo, bado zimeendelea kuishi katika hali ya uhasama,
chuki na wasi wasi wa kuweza kuzuka tena kwa vita.
Jumuiya ya Kimataifa ilishuhudia
madhara makubwa ya matumizi ya silaha za kinyuklia wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia,
lakini jambo la kushangaza ni kuona kwamba, bado kuna mashindano makubwa ya utengenezaji,
usambazaji na ulimbikizaji wa silaha za mahangamizi.
Wajumbe wa Baraza la
Makanisa Ulimwenguni katika mkutano wao wamesema, silaha za kinyuklia haziwezi kamwe
kuwa ni msingi wa amani mintarafu imani ya Kikristo. Wajumbe waliwakumbuka watu wote
wanaoendelea kuathirika kutokana na matumizi ya silaha za maangamizi kutoka sehemu
mbali bali za dunia.