2013-11-20 15:20:29

Siku ya Viwanda Barani Afrika na changamoto zake!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema Wizara ya Viwanda na Biashara haina budi kuwaendeleza wajasiriamali wenye viwanda vidogo na vya kati kwa kuwa vina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini. Ametoa kauli hiyo Jumatano, Novemba 20, 2013) wakati akizungumza na wenye viwanda na wajasiriamali mbalimbali wakati wa kuadhimisha Siku ya Viwanda Afrika iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Maonesho wa Mwalimu J.K. Nyerere, barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam.

Waziri Mku alisema sekta ya viwanda vidogo ina nafasi kubwa sana katika kukuza ajira, kuondoa umaskini, na kuongeza pato la mwananchi mmoja mmoja na imekuwa ikikua hatua kwa hatua. “Hivi sasa sekta hii ina viwanda vidogo vidogo zaidi ya milioni tatu ambavyo vinaajiri zaidi ya Watanzania milioni 5.2. Mchango wake katika Pato la Taifa ni asilimia 27 na kwenye ajira ni asilimia 23.4 ya nguvu kazi yote nchini”, alisema.

Alisema msukumo mkubwa uliowekwa na Serikali ya Awamu ya Nne katika kuendeleza viwanda ilikuwa ni pamoja na uanzishwaji na uendelezaji wa maeneo ya fursa huru za uwekezaji kama Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uzalishaji kwa mauzo Nje (EPZA) na Maeneo Maalum ya Uwekezaji (Special Economic Zones – SEZ).

“Serikali imechukua hatua mbalimbali katika kuimarisha ushiriki wa sekta binafsi katika uwekezaji na biashara katika soko la ushindani. Hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuipa nguvu ya kisheria Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uzalishaji kwa Mauzo Nje (EPZA) kusimamia uwekezaji katika Maeneo Maalum ya Uwekezaji (Special Economic Zones – SEZ). Katika maeneo hayo, wawekezaji wa sekta mbalimbali wataweza kuzalisha na kuuza bidhaa katika masoko ya ndani na nje ya nchi,” alisema Waziri Mkuu.

Kuhusu usimamizi katika uwekezaji, Waziri Mkuu alisema Serikali imeendelea kusimamia uwekezaji katika maeneo maalum ya uzalishaji ili kuharakisha maendeleo ya viwanda. “Uendelezaji wa maeneo ya EPZ na SEZ ni moja ya mikakati ya kukuza ajira, uwekezaji na uzalishaji viwandani. Mpango huu una maeneo 10 ambayo yameonyesha mafanikio makubwa yakiwa yameajiri wafanyakazi 27,000. Miradi yote itakapokamilika, inatarajia kuajiri wafanyakazi 273,581,” aliongeza.
Alisema katika kipindi cha miaka sita iliyopita EPZ imeanzisha viwanda 81 katika maeneo mbalimbali nchini na kwamba viwanda hivyo vimewekeza mtaji wa zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.12 na vimetoa ajira za moja kwa moja 27,000 na zisizo za moja kwa moja zaidi ya 80,000.
Alisema mauzo ya nje yamefikia Dola za Marekani milioni 700. Serikali inaendelea kuimarisha EPZ ili iweze kuwa kichocheo cha kukuza uchumi na kujenga ajira kupitia maendeleo ya viwanda.

Mapema akizungumza kabla ya kumkaribisha Waziri Mkuu, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda alisema sekta ya viwanda nchini bado inakua kwa kasi ndogo ikilinganishwa na nchi nyingine duniani.

“Sekta ya viwanda hapa nchini inakua kwa asilimia tisa wakati China sekta hiyo imekua kwa asilimia 40, Vietnam imekua kwa asilimi 20 na India imefikia asilimia 16,” alisema.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa pia na mwakilishi Mwakilishi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) Nchini, Bw. Emmanuel Kalenzi, Mwenyekiti wa CTI, Bw. Felix Mosha na Wawakilishi wa Jumuiya za Kimataifa.









All the contents on this site are copyrighted ©.