Siku ya kuwaombea wamonaki kupambwa na uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko
Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 21
Novemba 2013 majira ya jioni anatarajiwa kuwatembelea na kusali na Wamonaki Wacamaldoli
wa Mtakatifu Anthoni Abate, wanaoishi na kutekeleza utume wao mjini Roma. Itakuwa
ni fursa kwa Baba Mtakatifu kusali pamoja na wamonaki hawa, kama sehemu ya Maadhimisho
ya Siku ya Wamonaki, kama inavyojulikana kwa lugha ya Kilatini “Pro Orantibus”.
Ni
siku ambayo Mama Kanisa anaitumia kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea Wamonaki wanaojitosa
kwa sala, sadaka na tafakari ya kina ya Neno la Mungu katika hija ya maisha yao. Siku
kuu hii ilianzishwa kunako Mwaka 1953 na Papa Yohane wa Ishirini na tatu, aliyetangaza
kwamba, Kanisa katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, liwakumbuke
pia Wamonaki wanaojitoa bila ya kujibakiza kwa njia ya sala na tafakari ya kina kwa
ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Lakini itakumbukwa kwamba, Siku kuu ya Bikira
Maria kutolewa Hekaluni ilianzishwa na Papa Pio wa Kumi na mbili kunako tarehe 13
Mei 1953, siku maalum kwa ajili ya kusali na kuwaombea Wamonaki waliotawanyika sehemu
mbali mbali za dunia sanjari na kuwasaidia kwa hali na mali ili waweze kuendeleza
utume wao kwa Kristo na Kanisa lake. Hata kama miito ya maisha ya kuwekwa wakfu inachechemea,
lakini bado watawa wanayo nafasi na dhamana kubwa katika maisha na utume wa Kanisa.
Watawa wa ndani wana maisha tofauti kabisa, ni kundi linalopaswa kutiwa moyo.
Wamonaki
wa Camaldoli wanajiandaa kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko anasema
Mama mkuu Maria Michela Porcelato kwa furaha na moyo wa sala. Hili ni Shirika lililoanzishwa
kunako Karne ya kumi na nane na Mama Angela Maria Pezza, mjane aliyekuwa na watoto
watatu kwa kushirikiana na Watawa wa kiume Wacamaldoli wa Mtakatifu Gregori. Leo hii
watawa hawa wanatekeleza utume wao nchini: Italia, Tanzania, Polandi, Brazil na India.
Ni watawa wanaoipamba siku yao kwa sala, tafakari na kazi. Kuna kundi kubwa la waamini
kutoka Jimbo kuu la Roma wanaofika kwenye Monasteri hii kwa ajili ya kupata ushauri
wa maisha ya kiroho.