"Msipokuwa na imani thabiti mtatangatanga kama daladala iliyo katika usukani"!
Kardinali William Levada, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu
ya Kanisa katika tafakari yake juu ya Mwaka wa Imani kama sehemu ya Maadhimisho ya
Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekisimu Mpya
ya Kanisa Katoliki anasema, ilikuwa ni hamu na utashi wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, kuona kwamba, Mwaka wa Imani unawasaidia waamini kusoma na kupitia
tena Nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na Katekisimu Mpya
ya Kanisa Katoliki, nyaraka muhimu sana katika mabadiliko ya maisha na utume wa Kanisa.
Mwenyeheri
Yohane Paulo II alipokua anazungumza na Tume ya Makardinali waliokuwa wamepewa dhamana
ya kuandika Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki aliwakumbusha kwamba, Katekisimu hii
inapaswa kuwa ni chombo cha umoja na mshikamano katika imani; umoja ambao unapata
chimbuko lake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Katekisimu iwe ni muhtasari wa Imani,
Sakramenti, Maisha Adili na Sala ya Kanisa. Iwe ni mwongozo katika katekesi zinazotolewa
na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, kwa ajili ya Wakatekumeni.
Kardinali
Levada anakumbusha kwamba, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ni Kitabu cgha rejea
kwa Maaskofu waliopewa dhamana ya kufundisha imani, kuwaongozwa na kuwatakatifuza
Watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani. Ni kitabu muhimu kwa wadau wa
Uinjilishaji wanaomsaidia Askofu kutekeleza wajibu wake barabara. Hawa ni Makleri,
Watawa, Makatekista na Walimu wa dini shuleni.
Ni chombo na mwongozo kwa wahubiri
na kwa ajili ya waamini wote katika mchakato wa majiundo endelevu ya Familia ya Mungu;
kielelezo cha utofauti katika umoja katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo yaani
Kanisa. Hili ni Kanisa moja, Takatifu, Katoliki na la Mitume. Ni msingi wa utume na
maisha ya viongozi wa Kanisa katika ujumla wao. Mama Kanisa anawahitaji waamini walei
wanaoifahamu kwa kina na mapana imani: wanayoikiri kwa vinywa vyao; kuiadhimisha katika
matendo ya Kiliturujia na Kisakramenti; Imani inayojidhihirisha katika matendo adili
yanayoongozwa na Amri za Mungu; imani inayomwilishwa katika Sala na Matendo ya huruma.
Kumbe, ni dhamana ya Kanisa kuhakikisha kwamba, waamini wanafundishwa kikamilifu
juu ya Imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuweza kuwa na waamini ambao wako
tayari kujitosa kimasomaso kutolea ushuhuda wao kwa maneno, lakini zaidi kwa njia
ya matendo yao! Waamini wasipokuwa na imani thabiti, wataendelea kutangaza tanga kama
”daladala” iliyokatika usukani. Watashindwa kuwa ni chumvi na mwanga
wa dunia.
Ni mwaliko kwa Wakristo kuhakikisha kwamba, imani hii wanawarithisha
pia watoto wao kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, mlango na kitambulisho cha Mkristo.
Sakramenti zimewekwa ili kuwatakatifuza wanadamu; kulijenga Fumbo la Mwili wa Kristo,
yaani Kanisa na hatimaye, kumtolea Mwenyezi Mungu ibada. Hizi ni ishara zinazodai
imani inayomwilishwa katika ushuhuda na matendo adili. Waamini wajitahidi kuifahamu
Kanuni ya Imani kwa kichwa, kwani ni sehemu ya Uinjilishaji mpya na mchakato wa kuyatakatifuza
malimwengu.
Waamini waifahamu imani ya Kanisa na kuitolea ushuhuda; wawe na
ujasiri wa kuitetea pale inaposhambuliwa. Huu ni mchakato wa Familia ya Mungu katika
ujumla wake. Waamini wahakikishe kwamba, wana imarishwa kwa Sakramenti ya Kipaimara,
tayari kuwa kweli ni Maaskari amini wa Kristo; wawe tayari kuwasha moto wa Injili
kwa watu wenye kiu ya kusikia Neno la Mungu likitangazwa kwenye viunga na maeneo yao
ya kujidai!
Na kwa makala hii, leo tunafunga mfululizo wa tafakari ya kina
kuhusu Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican na Miaka 20 tangu Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki ilipochapishwa.
Ikumbukwe kwamba, kila mwaka ni mwaka wa imani, ndivyo Kardinali William Levada, Mwenyekiti
mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa anavyowatupia ”madongo”
waamini katika Kufunga Mwaka wa Imani.
Na Padre Richard A. Mjigwa,
C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.