Mapadre ambao kimsingi ni wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho wanahitaji kuonja upatanisho
na uponyaji!
Baba Mtakatifu Francisko, wakati wa katekesi yake, Jumatano tarehe 20 Novemba 2013
kama sehemu ya mwendelezo wa tafakari juu ya Kanuni ya Imani amegusia kipengele cha
"Ubatizo mmoja kwa maondoleo ya dhambi" na kuhusu "funguo" walizokabidhiwa Mitume
kwa ajili ya maondoleo ya dhambi. Roho Mtakatifu aliyewashukia Mitume baada ya Ufufuko
wa Kristo ndiye mhusika mkuu katika maondoleo ya dhambi na Kanisa likakabidhiwa dhamana
hii kuitunza.
Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, Kanisa ni mhudumu tu wa msamaha
unaotolewa na Kristo kwa njia ya Roho Mtakatifu. Kanisa linawasindikiza waamini katika
hija ya toba na wongofu wa ndani kwa maisha yao yote sanjari na kuwaalika kuonja tena
mang'amuzi ya upatanisho wenye mwelekeo wa Kijumuiya na Kikanisa. Msamaha huu unatolewa
kwa njia ya Padre.
Kwa njia ya utume wa Padre, Mwenyezi Mungu amewakirimia
waamini ndugu anayeweza kuwapatia msamaha wa dhambi kwa njia ya Kanisa. Mapadre ambao
kimsingi ni wahudumu wa Sakramenti ya Upatanisho watambue kwamba, hata wao wanahitaji
kuonja huruma na uponyaji na kwamba, ni utume wanaopaswa kuutekeleza kwa njia ya unyenyekevu
na huruma.
Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha waamini kwamba, kamwe Mwenyezi
Mungu hawezi kuchoka kuwapatia msamaha. Anawaalika waamini kuthamini Sakramenti ya
Upatanisho na kufurahia zawadi ya huruma na uponyaji inayopatikana kwa njia ya utume
unaotolewa na Mapadre. Kwa njia hii, waamini wanaweza kutembea kwa uaminifu kama wafuasi
wa Kristo.Amewaomba waamini na mahujaji kuendelea kusali kwa ajili yake na kwamba,
Yeye pia anasali kwa ajili yao!
Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu ametambua
uwepo wa Mapadre kutoka Polandi wanaotekeleza utume wao miongoni mwa wahamiaji na
wakimbizi kutoka Poland. Anasema, wahamiaji wanakabiliana na changamoto mbali mbali
katika maisha yao: wana wasi wasi mwingi, wanakabiliana na matatizo na hatari katika
maisha na wakati mwingine wanajikuta kwamba, wanakata mizizi na tamaduni na hata familia
zao.
Amewataka Mapadre hao kuwa mstari wa mbele ili kuwasaidia ndugu zao katika
maisha ya kiroho, ili waweze kutunza imani na daima wakiwa mashahidi wa Jamii wanamoishi.
Mwishoni, Baba Mtakatifu amewakumbuka kwa namna ya pekee wananchi wa Sardegna wanaokabiliana
na mafuriko.