2013-11-20 11:21:25

Kanisa linapenda kuwekeza katika huduma kwa wazee na wagonjwa kwa njia ya mikakati makini!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski akishirikiana na viongozi waandamizi kutoka Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mkutano wa kimataifa wa ishirini na nane unaoongozwa na kauli mbiu "Kanisa katika huduma ya wazee wagonjwa: tiba kwa wagonjwa walioathirika na magonjwa ya mishipa ya fahamu" anasema, wazee wanayo nafasi muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa na kamwe hawana mbadala.

Mkutano huu unaoanza Alhamisi tarehe 21 Novemba 2013 ni fursa ya: tafakari, majadiliano na sala ili kufanya maboresho ya huduma ya afya na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wazee wagonjwa na watu walioathirika kwa magonjwa ya mishipa ya fahamu. Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya ushuhuda wa maneno na matendo yake ameonesha umuhimu wa wazee na wagonjwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Wajumbe 700 kutoka katika nchi 57 duniani wanaoshiriki katika mkutano huu, inaonesha sanaa na utamaduni wa Mama Kanisa katika kusikiliza, kujadiliana na kueleweshana kama kielelezo cha Kanisa la kiulimwengu. Haya ni majadiliano endelevu kwa wale wanaopania kudumisha mchakato wa maboresho katika sekta ya afya, kwa kutambua kwamba, wahudumu katika sekta ya afya ni wasamaria wema wanaowaonjesha jirani zao huruma na upendo wa Mungu.

Askofu mkuu Zimowski anasema kuwa, huduma makini kwa wazee na wagonjwa ni sehemu ya utekelezaji wa haki msingi za binadamu. Kanisa halina budi kuwa na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wazee na kwamba, huduma hii ni sehemu ya Uinjilishaji unaozingatia mahitaji ya wazee kwa kuwashirikisha katika maisha na utume wa Kanisa. Wazee waonjeshwe mshikamano wa upendo kutoka kwa vijana; wathaminiwe na kupendwa na kwamba, kila mmoja wao amenuiwa, akapendwa na hatimaye, akaumbwa na Mwenyezi Mungu na kwamba, kila mtu ni muhimu na wala hakuna mbadala!

Monsinyo Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anasema kwamba, mabingwa walioteuliwa na baraza lake la kipapa wanaonesha msukumo wa pekee unaotolewa na Mama Kanisa kwa ajili ya wazee wagonjwa, ambao wanapaswa kupewa uangalizi maalum, ili waendelee kuchangia katika maendeleo na ustawi wa Jamii na Kanisa katika ujumla wake.

Wagonjwa wa mishipa ya fahamu wanaendelea kuongezeka siku hadi siku, hali ambayo inaleta changamoto kubwa katika kupanga mikakati ya kiuchumi na shughuli za kichungaji kwa ajili ya wagonjwa hawa. Serikali na Jumuiya ya Kimataifa kwa ujumla wanapaswa kuliona tatizo hili na kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana nalo.

Kwa upande wake, Dr. Gabriele Carbone anasema, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa na matumaini ya wagonjwa hawa kupata nafuu, ikiwa kama itawekeza katika tafiti ili kudhibiti athari za magonjwa haya sanjari na kuanza mchakato wa maboresho ya maisha ya wagonjwa, jambo linalohitaji mtaji mkubwa. Kiasi cha dolla za kimarekani billioni 604 zinatumika kwa ajili ya kupambana na magonjwa sehemu mbali mbali za dunia, sawa na asilimia moja ya pato ghafi la nchi nyingi duniani. Familia nyingi zinaendelea kuteseka kwa kuwahudumia wazee wagonjwa, kumbe, maboresho ya tiba na huduma kwa wazee ni jambo linaloweza kuleta nafuu katika maisha ya familia nyingi.

Kwa upande wake, Padre Augusto Chendi, Katibu mkuu msaidizi anasema, ushuhuda unaoendelea kutolewa na Baba Mtakatifu Francisko kwa wagonjwa na wazee ni jambo la kutia moyo na changamoto inayopania kuibua mikakati ya shughuli za kichungaji kwa ajili ya wazee na wagonjwa; kwa kuwashirikisha katika maisha ya sala, toba na utume wa Kanisa kwani wao bado ni wadau wakuu katika utume na maisha ya Kanisa.







All the contents on this site are copyrighted ©.