2013-11-20 14:48:01

Familia iwe ni kielelezo cha udugu, umoja na mshikamano unaoguswa na mahitaji ya kila mtu!


Baba Mtakatifu Francisko anasema, tarehe 21 Novemba 2013, Mama Kanisa anaadhimisha Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni sanjari na Maadhimisho ya Siku kuu ya Kuwaombea Wamonaki. Hii ni fursa makini kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa watawa wanaotolea maisha yao kwa Mungu kwa njia ya sala na ukimya tendaji!

Kwa niaba ya Kanisa, Baba Mtakatifu anawashukuru Wamonaki kwa ushuhuda wa maisha wanayotolea; anawataka waamini kuwasaidia kwa hali na mali ili waweze kutekeleza utume wao kikamilifu.

Baba Mtakatifu anasema, kwamba, tarehe 22 Novemba 2013, Umoja wa Mataifa utazindua rasmi Maadhimisho ya Mwaka wa Kimataifa wa Familia Vijijini. Anaiomba Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inawajengea uwezo wa kiuchumi wakulima vijijini ili waweze kuwa kweli ni watu wanaoheshimu kazi ya uumbaji makini kwa mahitaji yao msingi.

Hata katika mazingira ya kazi, familia ni kielelezo cha udugu, umoja na mshikamano unaohitaji kwa namna ya pekee kuguswa na mahitaji ya kila mtu ndani ya familia husika pamoja na kuepuka kinzani za kijamii zinazoweza kujitokeza. Baba Mtakatifu anapongeza juhudi hizi na anatumaini kwamba, zitasaidia mchakato wa kukuza shughuli za kiuchumi, kijamii, kitamaduni na kimaadili kwa ajili ya Jumuiya ya binadamu.







All the contents on this site are copyrighted ©.