Wazee ni hazina ya Jamii, waheshimiwe na kutunzwa!
Jamii inapaswa kuwaheshimu na kuwaenzi wazee kwani hawa ni maktaba hai inayoiwezesha
Jamii kurithisha tunu bora za maisha ya kiroho na kiutu; mapokeo na tamaduni njema
kutoka kizazi kimoja hadi kingine kama alivyofanya Eliezari shahidi anayesimuliwa
kwenye Kitabu cha Kwanza cha Wamakabayo.
Ni shahidi aliyethubu kukabiliana
na kifo dini kuliko kudanganya kuhusu Sheria na Amri za Mungu, akalijitahidi kuwa
mwaminifu kwa Mungu na Jamii hadi dakika ya mwisho wa maisha yake na wala vitisho
vya kifo havikumtia wasi wasi, bali alitamani kuwaachia vijana urithi utakaodumu katika
maisha yao! Alihisi dhamana kubwa iliyokuwa mbele yake kama Mzee katika Jamii na mfano
wa kuigwa na vijana wa kizazi kipya katika imani na maisha adili. Ni mfano unaoweza
kutolewa na mashahidi wa kila siku katika familia! Wazee waheshimiwe na kamwe si watu
wa kubezwa na kutengwa!
Ni changamoto iliyotolewa na Baba Mtakatifu Francisko,
Jumanne, tarehe 19 Novemba 2013 wakati wa Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye
Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican. Baba Mtakatifu anasema, wazee
ni watu waliotangaza Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao, wakajitahidi
kuwa waaminifu kwa Neno la Mungu na maisha adili. Inasikitisha kuona wazee wengi wakikabiliwa
na magonjwa na hali ya kukata na kukatishwa tamaa. Ni wazee ambao wengi wao wametelekezwa
kwenye nyumba za wazee na hospitalini, lakini ikumbukwe kwamba, wazee ni hazina ya
Jamii.
Hawa ni mashahidi wa imani, waliovumilia madhulumu, wakawa tayari kurithisha
imani yao kwa vijana wa kizazi kipya. Jambo la msingi ni Jamii kuendelea kuwa na huruma
na mapendo kwa wazee, kwa kuwasikiliza na kuwahudumia kwa moyo mkuu na unyenyekevu.