2013-11-19 12:23:44

Wasaidieni wahamiaji kutambua: utamaduni, mila na desturi zao, ili kumwilisha tunu za Kiinjili mahali wanapoishi!


Historia ya Poland imefumbata pamoja na mambo mengine matukio yaliyopelekea wananchi wengi wa Poland kuikimbia nchi yao. Hali hii iliwakumbuka hata waamini wa Kanisa Katoliki, hali ambayo ililihamasisha Kanisa kuibua mbinu mkakati kwa ajili ya kuwahudumia wahamiaji na wakimbizi waliokuwa wanaishi ugenini.

Huu ukawa ni mwanzo wa Mapadre wa kiroho wanaojitoa kwa ajili ya wakimbizi pamoja na wahamiaji katika hija ya maisha yao ya kila siku. Mapadre wanaowahudumia wahamiaji na wakimbizi wanatekeleza dhamana na utume wao kama Mashemasi wa huduma ya umoja na mshikamano. Wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanalinda na kudumisha utambulisho wa mahali wanapotoka wahamiaji na wakimbizi kwa kuzingatia: tamaduni, mila, desturi na ibada zao.

Wana wajibu wa kuwasaidia kujishikamanisha na Jamii inayowazunguka pamoja na Kanisa mahalia. Kwa njia hii, wahamiaji na wageni wanaweza pia kumwilisha ndani mwao ari na moyo wa kimissionari tayari kujitosa kimasomaso kwa ajili ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao hata wanapokuwa ugenini!

Ni maneno yaliyotolewa na Kardinali Antonio Maria VegliĆ², Rais wa Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum wakati wa hija yao ya kichungaji mjini Roma, kuanzia tarehe 19 hadi tarehe 21 Novemba 2013.







All the contents on this site are copyrighted ©.