Tarehe 24 Novemba 2013 Papa kukabidhi Waraka wa "Furaha ya Injili" kwa waamini kama
sehemu ya kufunga Mwaka wa Imani
Baba Mtakatifu Francisko katika kilele cha Maadhimisho ya Mwaka wa Imani sanjari na
Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu anatarajiwa kuwakabidhi waamini Waraka
Mpya wa Kichungaji, "Evangelii Gaudium" Yaani "Furaha ya Injili" kama alama ya kudumu
ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Ibada ya Misa inatarajiwa kuanza saa 4:30 kwa saa
za Ulaya.
Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Rino Fisichella, Rais wa Baraza la
Kipapa la Uhamasishaji wa Uinjilishaji mpya alipokuwa anazungumza na vyombo vya habari
mjini Vatican siku ya Jumatatu, tarehe 18 Novemba 2013. Mkutano huu umehudhuriwa pia
na viongozi waandamizi kutoka Baraza hili.
Tukio la Baba Mtakatifu Francisko
kuwakabidhi waamini Waraka Mpya wa Kichungaji ndicho kiini cha Maadhimisho ya Kufunga
Mwaka wa Imani, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Wawakilishi 36
kutoka katika nchi 18, watapewa dhamana ya kutangaza yaliyomo kwenye Waraka wa Furaha
ya Imani, kwa kutambua kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wanapewa dhamana
ya kutangaza Injili ya Kristo kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao hadi miisho ya dunia.
Waraka huu watakabidhiwa: Askofu kutoka Lituania, Padre mmoja kutoka Tanzania na Shemasi
kutoka Australia.
Baba Mtakatifu Francisko pia atawakabidhi Waraka huu Watawa
wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kichungaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia, walioshiriki
kwa namna ya pekee kabisa kupamba Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, bila kuwasahau wasanii
wanaoshiriki kikamilifu katika dhamana ya Uinjilishaji kwa njia ya karama na vipaji
vyao. Kati ya waamini 36, wapo pia waandishi wa habari wawili watakaokabidhiwa dhamana
ya kushiriki katika azma ya Utangazaji Injili, kwani Mama Kanisa anautambua mchango
wao makini anasema Askofu mkuu Fisichella.
Waamini kwa mara ya kwanza katika
historia ya Kanisa, wataweza kutoa heshima yao kwa masalia yanayosadikiwa kuwa ni
ya Mtakatifu Petro, aliyeitwa kuwaimarisha ndugu zake katika imani, akasimama kidete
kuitetea kwa njia ya ushuhuda wa maisha yake. Katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
watu zaidi ya millioni 8. 5 wametembelea na kukiri Kanuni ya Imani kwenye Kanisa kuu
la Mtakatifu Petro, mjini Vatican.