Sheria mpya kuhusu fedha yapitishwa na Papa Francisko
Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 14 Novemba 2013 alitia sahihi barua ya kitume
iliyopitisha Katiba na Sheria za Mamlaka ya Intelijensia ya Fedha, (F.I.A.), ambazo
zitaanza kutumika tarehe 21 Novemba 2013. Ni sheria ambazo zinakazia pamoja na mambo
mengine kuhusu: ukweli na uwazi, Usimamizi na intelijensia katika masuala ya fedha.
Baba Mtakatifu ameimarisha sheria hizi kwa ajili ya mji wa Vatican ili kuhakikisha
kwamba, shughuli za fedha zinazingatia sheria, kanuni na maadili kama inavyotakiwa.
Baba Mtakatifu Francisko amefanya maboresho kwenye sheria zilizokuwa zimekwisha idhinishwa
na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, hapo tarehe 30 Desemba 2010 kwa kutaka wadau
kutekeleza dhamana hii nyeti kwa kuzingatia kanuni, maadili, weledi na taaluma yao.
Sheria mpya inafafanua dhamana na majukumu ya Rais, Bodi ya Wakurugenzi na
Uongozi ili kuhakikisha kwamba, Mamlaka ya Intelijensia inafanya kazi zake barabara.