Je, bado waamini mna mwamko wa kutaka kujifunza Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki?
Kardinali William Levada, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu
ya Kanisa katika tafakari yake juu ya Mwaka wa Imani kama sehemu ya Maadhimisho ya
Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na Miaka 20 ya Katekisimu Mpya
ya Kanisa Katoliki anasema kuna uhusiano wa dhati kati ya Mwaraka wa kichungaji: Mlango
wa Imani na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki.
Mwanzoni mwa
Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican ilionekana kana kwamba, hakuna umuhimu
wa kuwa na Katekisimu ya Kanisa Katoliki na kwamba, Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican zilikuwa zinajitosheleza.
Lakini baadaye, waamini walikumbushwa
kwamba, Mwenyezi Mungu alimpatia mwanadamu Amri kumi na wala si ushauri wa maisha
ya kiroho na kimaadili, kumbe kulikuwa kuna haja ya kuwa na Katekisimu Mpya ya Kanisa
Katoliki na Muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa: Hizi ni nyaraka zinazofundisha
imani na maadili kwa kufumbata Maandiko Matakatifu na Liturujia ya Kanisa kwa ajili
ya watu wa kizazi kipya.
Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, kunako Mwaka 1985
mara baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu akaamua kuufanyia kazi ushauri wa
Mababa wa Sinodi kwa kuanzisha mchakato wa kutunga Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki,
dhamana aliyopewa Kardinali Joseph Ratzinger kwa wakati huo. Akashirikiana na Tume
ya Makardinali 12.
Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi
na teknolijia, ulimwengu unaonekana kuwa kama kijiji. Kumbe kutokana na changamoto
hizi, kulikuwa na haja kwa Kanisa kuwa muundo wazi unaonesha umoja na mshikamano katika
maisha ya kiroho kwa kuwa na: sheria za pamoja, Katekisimu kwa ajili ya Kanisa zima,
Alama za Kiliturujia na mambo msingi katika shughuli za kichungaji. Kardinali Levada
anasema kwamba, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki inasimikwa katika misingi mikuu
minne ya maisha na utume wa Kanisa: Ni muhtasari wa imani inayoungamwa kwenye Kanuni
ya Imani; Imani inayoadhimishwa kwenye Liturujia na Sakramenti za Kanisa; Imani inayomwilishwa
katika uhalisia wa maisha kwa njia ya neema na Baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu mintarafu
Amri kumi za Mungu na kwamba, hii ni imani inayowasukuma waamini kusali na kuimwilisha
katika matendo ya huruma.
Kwa maneno mengine, Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki
ni muhimu sana katika maisha ya Kanisa na utume wa Makatekista; ni chachu ya mageuzi
na chombo cha kufundishia imani. Katekisimu ni muhtasari wa imani ya Kanisa iliyorithishwa
kutoka katika Maandiko Matakatifu, ikafundishwa na Mababa wa Kanisa na Kumwilishwa
na watakatifu pamoja na Wamissionari katika maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali
mbali za dunia.
Kwa hakika anasema Mwenyeheri Yohane Paulo wa Pili, Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki ni utajiri wa Kaniza zima. Katekisimu hii ilipotolewa kwa
mara ya kwanza, watu wengi waliinunua. Je, baada ya miaka 20 tangu kuchapishwa kwake,
waamini na watu wenye mapenzi mema bado wana ari na mwamko wa kutaka kujifunza yaliyomo
kwenye Katekisimu hii? Naam, usikose kujiunga nasi tena, tutakapoendelea kukuletea
tafakari ya kina kutoka kwa Kardinali William Levada wakati huu Mama Kanisa anapofunga
Mwaka wa Imani. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.