2013-11-19 12:22:31

Huduma ya Kanisa kwa wazee na wagonjwa!


Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anasema, kwamba, mkutano wa ishirini na nane wa Baraza lake utakaoongozwa na kauli mbiu “Kanisa katika huduma kwa wazee wagonjwa: tiba kwa wagonjwa walioathirika na magonjwa ya mishipa ya fahamu” ni mada inayopania kupembua kwa kina na mapana athari zinazosababishwa na magonjwa haya katika karne ya ishirini na moja.

Wataalam wa afya ya binadamu wanasema, haya ni kati ya magonjwa yanayoendelea kusababisha vifo na mateso makubwa kwa wazee sehemu mbali mbali za dunia.

Mkutano huu utakaohudhuriwa na wajumbe 400 kutoka sehemu mbali mbali za dunia, unatarajiwa kufunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu Alhamisi, tarehe 21 Novemba na kufungwa kwa tafakari ya kina itakayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko, hapo tarehe 23 Novemba 2013.

Askofu mkuu Zygmunt Zimowski anasema kwamba, mkutano huu unafanyika kwa utashi ulioneshwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kuwasaidia wazee na watu wenye umri mkubwa katika mchakato wa mapambano dhidi ya magonjwa sanjari na kuwapatia wazee kipaumbele wanachostahili. Haki ya afya kwa wazee wagonjwa ni jambo la muhimu sana katika Jamii pamoja na kuhakikisha kwamba, wazee wanapewa matunzo na heshima wanayostahili kwa kushirikishwa katika maisha ya Jamii husika kadiri ya hali zao.

Wazee ni hazina kubwa ya hekima na tunu bora za maisha ya kijamii, ikiwa kama watatumiwa kikamilifu, lakini uzoefu unaonesha kwamba, wazee katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi hawana nafasi tena, kwani wanaweka “kiwingu” kwa watu wengine ndani ya Jamii kufurahia maisha.

Takwimu zinaonesha kwamba, duniani kuna zaidi ya watu millioni 36 walioathirika kutokana na magonjwa ya mishipa ya fahamu kutokana na uzee. Hadi kufikia mwaka 2050 inasadikiwa kwamba, idadi hii inaweza kuongezeka maradufu, ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa haitachukua hatua za makusudi kupambana na magonjwa ya mishipa ya fahamu yanayoendelea kusababisha mateso makali kwa wazee na watu wenye umri mkubwa.

Huduma zinazotolewa kwa wagonjwa hawa Hospitalini inaonekana kana kwamba, bado hazijaweza kufua dafu, anasema Askofu mkuu Zymowski, hata katika nchi ambazo Serikali zimewekeza zaidi katika maboresho ya sekta ya afya. Tija na ufanisi mkubwa vinaweza kupatikana kwa wagonjwa hawa kuhudumiwa katika maeneo yao kwa kukazia kwanza kabisa: uchunguzi wa kina na tiba muafaka bila kusahau huduma za kitabibu zinazopaswa kutolewa kwa wagonjwa kama hawa.

Wataalam, watafiti na mabingwa wa magonjwa ya mishipa ya fahamu kutoka sehemu mbali mbali za dunia, kwa muda wa siku tatu watakuwa mjini Vatican kubadilishana uzoefu na mang’amuzi katika huduma kwa wazee wanaokabiliwa na magonjwa ya mishipa ya fahamu. Wajumbe watashirikisha mikakati na sera makini zinazoweza kusaidia maboresho ya huduma ya afya kwa wagonjwa.

Itakumbukwa kwamba, Kanisa Katoliki liko mstari wa mbele katika huduma za kiafya na wazee wamekuwa wakipatiwa huduma msingi kutoka katika taasisi zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa, hapa wajumbe wataangalia taalimungu na mikakati ya kichungaji kwa ajili ya wazee wagonjwa, ili kuwajengea imani, matumaini na mapendo, kwani hata katika uzee na magonjwa yao, Kanisa bado linaendelea kuwathamini na linataka kuwaenzi.








All the contents on this site are copyrighted ©.