2013-11-18 09:36:14

Yatakayojiri wakati wa kufunga Mwaka wa Imani: Sherehe ya Kristo Mfalme


Mama Kanisa anajiandaa kufunga rasmi Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita na kuendelezwa kwa ari na moyo mkuu na Papa Francisko hapo tarehe 24 Novemba 2013, wakati wa Sherehe ya Kristo Mfalme. Ibada hii inatarajiwa kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa saa za Ulaya. Maadhimisho ya kufunga Mwaka wa Imani yataanza rasmi kwa tafakari ya kina kuhusu maisha ya watawa wa ndani, hapo tarehe 21 Novemba 2013, siku ambayo Mama Kanisa anawakumbuka na kuwaombea watawa wa ndani.

Hii ni Siku kuu ya Bikira Maria kutolewa Hekaluni, ambayo kimsingi utakuwa ni mwanzo wa Maadhimisho ya hitimisho la Mwaka wa Imani. Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Wakatekumeni, Jumamosi, tarehe 23 Novemba 2013 na tarehe 24 Novemba, 2013, itakuwa ni Misa ya kufunga Mwaka wa Imani.

Jumamosi, tarehe 23 Novemba 2013 Baba Mtakatifu atakutana na Wakatekumeni ambao wamekutana na Kristo wakiwa katika umri mkubwa, wakaonja furaha ya imani na hatimaye, kuamua kubatizwa na kuwa ni wafuasi wa Kristo. Hii itakuwa ni alama ya imani katika kufunga Mwaka wa Imani, lakini bado waamini wanachangamotishwa kuendeleza matunda ya Mwaka wa Imani ambayo wamebahatika kuvuna wakati wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Wakristo wanahimizwa kupokea mwaliko na wito kutoka kwa Kristo ili waendelee kuwa wafuasi wake waaminifu, kwa kutolea ushuhda wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Kwa Sakramenti ya Ubatizo wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Kristo anawawahimiza kuwa ni mashahidi wa furaha inayobubujika kwa kukutana na Kristo katika hija ya maisha yao hapa duniani. Itakuwa ni fursa nyingine kwa Makatekista wanaowasindikiza Wakatekumeni katika majiundo yao ya Kikristo, kukutana tena na Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani.

Makatekista na Wakatekumeni hawa ni wale wanaotoka Jimbo kuu la Roma na viunga vyake. Ibada hii itaanza kwa Liturujia ya Neno la Mungu na baadaye kufuatiwa na Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu maana ya maisha mapya katika Kristo mintarafu Injili ya Yohane 1:35-42.

Baadhi ya Wakatekumeni watapokelewa rasmi na Baba Mtakatifu katika Ibada hii ya Liturujia ya Neno la Mungu. Hiki ni kikundi cha Wakatekumeni 10 ambao wamefuata katekesi kutoka katika Parokia mbali mbali za Jimbo kuu la Roma. Huu ni mchanganyiko wa Wakatekumeni: 3 ni Waitaliani, 2 kutoka Albania, 1 ni Mchina, 1 Mcuba, 1 Mmisri, 1 Mfaransa na 1 kutoka Lituania.








All the contents on this site are copyrighted ©.