2013-11-18 09:43:21

"Msiwe Wakristo wa Part Time tu"


Waamini walei wanapaswa kusimama kidete kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wa maisha yao kwa Kristo na Kanisa lake; wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini walei wawe makini kuendeleza tunu msingi za maisha ya ndoa na famia, taasisi ambazo kwa sasa zinakabiliwa na changamoto nyingi kutoka katika medani mbali mbali za maisha.

Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kushiriki kikamilifu katika maisha ya hadhara kwa njia ya ushuhuda makini, ili waweze kuwa kweli ni chumvi na mwanga wa mataifa, wakiongozwa na Kweli za Kiinjili sanjari na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Waamini watambue kwamba, wanao mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa kama walivyobainisha Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kimsingi, waamini walei wanatumwa ulimwenguni kwa njia ya maisha yao adili na manyofu, kuyatakatifuza malimwengu kwa harufu nzuri ya imani, matumaini na mapendo.

Huu ni mchango wa Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la Walei wakati alipokuwa anazungmza kwenye Kongamano la Kitaifa la Ishirini na sita la Wanasheria Wakatoliki nchini Ufaransa hivi karibuni. Anasema, inasikitisha kuona kwamba, kasi ya ukanimungu inaongezeka kwa kasi ya ajabu kiasi kwamba, Mwenyezi Mungu si rejea ya maisha na vipaumbele vya watu wengi duniani. Misimamo mikali ya imani na madhulumu dhidi ya Kanisa yanaongezeka maradufu, kiasi cha kutisha haki ya uhuru wa kidini.

Hizi ni changamoto na mwaliko kwa Makleri na Waamini walei kutoka huko walikojificha na kujimwaga katika ulimwengu kwa njia ya ushuhuda amini wa imani yao kwa Kristo na Kanisa lake, ili watu wa mataifa waweze kuonja tena utamu na uzuri wa kweli za Kiinjili, daima wakijitahidi kuwa ni chumvi na mwanga wa dunia na kwamba, wanao mchango mkubwa kwa ustawi na maendeleo ya watu: kiroho na kimwili, dhamana inayotekelezwa kwa njia ya Uinjilishaji. Kanisa na Serikali ni taasisi mbili zenye malengo taofauti, lakini zinaweza kushirikiana kwa ajili ya huduma na mafao ya wengi; kwa kuwa na mwono sahihi wa mtu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kama wanasheria, wanao mchango mkubwa katika maisha ya wananchi wengi wa Ufaransa, kwani wao ni wadau wakuu katika utunzi wa sheria na utekelezaji wake hasa katika ulimwengu mamboleo ambao ubinafsi unashika kasi ya ajabu, dhidi ya sheria asilia kuhusu ndoa na familia. Sheria za ndoa za watu wa jinsia moja zinazohamishwa kwa wingi sehemu mbali mbali za dunia, ni kielelezo cha kumong’onyoka kwa tunu msingi za kimaadili kwa kisingizio cha uhuru binafsi. Kama Waamini, wanaalikwa kusimama kidete kulinda na kutetea: utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Kamwe waamini wasiwe ni “Wakristo wa Part Time” kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, kwani Kanisa linawahitaji waamini amini, waliokomaa na kwamba, wako tayari kujitosa kimasomaso kutolea ushuhuda wa Injili kwa Kristo na Kanisa lake, wakijitahidi kumwilisha ndani mwao neema ya Sakramenti ya Ubatizo, inayowapatia dhamana na wajibu wa kutekeleza ndani ya Kanisa na Jamii inayowazunguka.

Haitoshi kuitwa Mkristo, bali inatakiwa kweli kuwa ni Mkristo kwa maneno, lakini zaidi kwa njia ya ushuhuda wa matendo amini na makini, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Mungu, Kristo, Kanisa na Jirani. Waamini wawe ni mashahidi wa imani wanayokiri, adhimisha, ishi na kusali, changamoto wakati huu wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema kwamba, ikiwa kama Muumba hataheshimiwa, kiumbe chake kiko mashakani.

Kardinali Rylko anasema, athari za myumbo wa uchumi kimataifa zinazojionesha katika mmong’onyoko wa kimaadili na utu wema, zinaweza kuwatumbukiza waamini katika hali ya kuchanganyikiwa na kukata tamaa. Hapa jambo la msingi ni kuendelea kuwa na matumaini, kila mwamini akijitahidi kutekeleza wajibu wake. Kamwe, waamini wasiwaruhusu wajanja wachache kuwapokonya matumaini yao, bali wajitahidi kusoma alama za nyakati na kuwa makini zaidi. Kinzani na myumbo wa maisha adili ni fursa makini ya kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu; mwanadamu akipewa msukumo wa pekee.

Waamini wanakabiliana na changamoto kutoka katika medani mbalimbali za maisha. Wakristo kwa sasa wanaweza kufanishwa na sauti ya mtu aliyeaye nyikani; sauti ambayo hakuna anayeisikiliza wala kuithamini, ni sawa na “kelele za chura ambazo hazimnyimi ng’ombe kunywa maji”! Lakini, hata katika mmong’onyoko wa kimaadili, bado watu wanaendelea kujenga na kuimarisha dhamiri nyofu, kwa kutambua mema yakufuata na mabaya yakuachana nayo!

Ndiyo maana kuna watu bado wanaendelea kusimama kidete kulinda na kutetea tunu msingi za maisha ya ndoa na familia kama wanavyofanya waamini na watu wengi wenye mapenzi nchini Ufaransa. Dhamana na utume wa waamini walei ni kuendelea kuwa ni chumvi na mwanga wa mataifa kama kikolezo cha kuyatakatifuza malimwengu.








All the contents on this site are copyrighted ©.