2013-11-18 09:10:03

Msikubali kudanganywa kuhusu vitimbwi vya mwisho wa dunia! Bali iweni watu wa imani na saburi!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Jumapili tarehe 17 Novemba 2013 kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, amewataka waamini na watu wenye mapenzi mema, kuwa makini na kamwe wasikubali kudanganywa kuhusu mwisho wa dunia kwani, kuna wengi watakuja kwa jina la Yesu na katu, wasikubali kuingiwa na hofu isiyokuwa na msingi.

Waamini wanaalikwa kuishi kipindi hiki cha kumngoja Bwana atakapokuja kuwahukumu wazima na wafu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji na udumifu katika maisha ya Kikristo. Waamini wa nyakati hizi wanaishi kipindi hiki cha kumngoja Bwana.

Baba Mtakatifu ameuambia umati mkubwa wa waamini na mahujaji uliofurika kwenye viunga vya Kanisa kuu la Mtakatifu Petro kwamba, hata waamini wanaoishi katika Karne ya Ishirini na Moja, bado wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutodanganyika kwa watu wanaojidai kuja kwa jina lake. Ni mwaliko kutambua Roho ya Kristo na kuifuata.

Hata leo hii anasema Baba Mtakatifu kuna "Wakombozi uchwara" wanaojitahidi usiku na mchana kutaka kuchukua nafasi ya Yesu Kristo, hao ni viongozi wa mambo ya kidunia, "mbwa mwitu waliovikwa ngozi ya mwanakondoo" na hata wachawi wanaotaka kujikweza kwa watu ili akili na mioyo yao ivutike kwao. Onyo, kamwe waamini wasikubali kuwafuata watu hao!

Kwa wale wanaomtumainia Kristo anawajalia pia neema na nguvu ya kushinda hofu hata pale wanapokabiliana na vita, mapinduzi, majanga asilia, na mlipuko ya magonjwa; Yesu anawakomboa kwa mambo yote haya na hivyo kuwa na mwono sahihi.

Baba Mtakatifu anasema, kama Wakristo watakabiliana na madhulumu pamoja na nyanyaso kwa ajili ya jina lake, lakini hata unywele mmoja wa vichwa vyao hautapotea, kwani wanapata tunza na hifadhi kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Madhulumu, nyanyaso na mateso wanayokabiliana nayo waamini ni nafasi ya kushuhudia imani yao na kujenga mshikamano wa dhati na Kristo na kamwe isiwe ni sababu ya kuwatenga na upendo wa Kristo.

Baba Mtakatifu amewakumbuka maelfu ya Wakristo wanaoteseka sehemu mbali mbali za dunia kutoka na imani yao kwa Kristo na Kanisa lake na kamwe wasijisikie pweke kwani Kanisa liko daima pamoja nao! Amewapongeza wote wanaoendelea kutolea ushuhuda wa imani tendaji bila wasi wasi wala woga kwani udumifu wao utawakirimia wokovu wa maisha!

Ni vyema ikiwa kama waamini watakuza ndani mwao fadhila ya matumaini na uvumilivu, wakisubiri kwa imani maisha ya uzima wa milele, kwani Mwenyezi Mungu ndiye kinara wa historia, yote yanapata hitimisho katika mpango wake. Licha ya magumu na matatizo yanayoweza kujitokeza ulimwenguni, lakini utashi na huruma ya Mungu kamwe haitaweza kutoweka, haya ndiyo matumaini ya Wakristo.







All the contents on this site are copyrighted ©.