2013-11-18 07:41:01

Mshikamano unahitajika katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na magonjwa!


Baraza la Maaskofu Katoliki India linasema kwamba, Kanisa haliwezi kukaa pembeni na kuwa mtazamaji katika mchakato wa mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi nchini India, bali linapaswa kusimama kidete kuchangia kwa hali na ubora wa maisha na mafao ya wengi. RealAudioMP3

Kanisa litaendelea kujihusisha na huduma za kijamii katika sekta ya elimu, afya na maendeleo endelevu kama sehemu ya changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa Uinjilishaji mpya. Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Hii ni kati ya mikakati iliyobainishwa na Baraza la Maaskofu Katoliki India hivi karibuni kama sehemu ya kongamano katika kufunga Mwaka wa Imani, ambao umekuwa ni fursa makini kwa waamini kujifunza tena nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na umuhimu wa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Mkusanyo wa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika maisha na utume wa Kanisa. Jumla ya wawakilishi 550 kutoka katika Majimbo 44 yanayounda kimsingi Baraza la Maaskofu Katoliki India wamehudhuria.

Kwa pamoja wamechangamotishana kuendelea kuwa ni alama na sauti ya kinabii kwa kushuhudia kweli za Kiinjili katika maisha na utume wa Kanisa, nchini India, daima wakiwa mstari wa mbele kupambana na umaskini katika nchi kubwa kama India yenye mazuri na magumu yake! Kuna kasi kubwa ya ukuaji wa kiuchumi nchini India, lakini pia kuna ongezeko la watu wanaoendelea kutumbukia na kutumbukizwa katika janga la umaskini wa hali na kipato. Takwimu zinaonesha kwamba, India ina idadi kubwa ya watu wanaoshambuliwa na baa la njaa kila mwaka.

Wajumbe kwa mara nyingine tena wameamua kumwilisha ujumbe na changamioto kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linashikamana na maskini, ili kuwasaidia maskini kuondokana na umaskini wao kwa kuwa na mikakati bora ya maisha inayojionesha katika shughuli za kichungaji zinazofanywa na Mama Kanisa nchini India. Umaskini unaweza kuondolewa nchini India kwa kuwekeza zaidi katika sekta ya elimu pamoja na kuendelea kuimarisha huduma zinazotolewa na Taasisi za Elimu Katoliki India.

Kanisa liwahamasishe watu kujenga na kuimarisha utamaduni wa mshikamano wa upendo, kwa kujali na kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao badala ya watu wachache ndani ya Jamii kuendelea kuneemeka kutoka na utajiri, rasilimali na fursa mbali mbali zinazopatikana nchini India. Inasikitisha kuona kwamba, watu wanaendelea kujikita katika utandawazi usiojali wengine.

Kanisa Katoliki nchini India kwa njia ya ushuhuda wa maisha na utume wake, liendelee kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa, ubadhirifu wa mali ya umma na ufisadi unaojengeka kwa kasi ya ajabu kwa kuendekeza mno ubinafsi.

Kanisa lisimame kidete dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kutangaza Injili ya Uhai, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake, hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango na mapenzi ya Mungu. Jamii inapaswa kuwalinda na kuwatetea wanyonge na wasiokuwa na sauti! Kwa namna hii, Kanisa Katoliki nchini India, litaendelea kumwilisha matunda ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani kwa sasa na kwa siku za usoni!








All the contents on this site are copyrighted ©.