2013-11-18 08:01:53

Jengeni Maktaba ili ziweze kuwa ni vituo vya rejea kwa wasomi!


Waziri mkuu wa Tanzania Mizengo Pinda amesema kila Halmashauri nchini Tanzania inapaswa kuweka kwenye mpango wake wa maendeleo kifungu cha ujenzi wa maktaba ya wilaya ili watu waweze kusoma na kujiendeleza kwa urahisi. Ametoa kauli hiyo Novemba 16, 2013) wakati akiwahutubia washiriki wa mahafali ya 19 ya Chuo cha Ukutubi na Uhifadhi wa Nyaraka cha Bagamoyo yaliyofanyika kwenye viwanja vya chuo hicho nje kidogo ya mji wa Bagamoyo.

Jumla ya wahitimu 749 walitunukiwa vyeti kati yao 244 vikiwa ni vya stashahada na 505 ni vya astahada katika fani za ukutubi na utunzaji nyaraka.

Alisema ukutubi ni mojawapo ya fani kongwe hapa duniani japo haiongelewi sana hapa nchini. “Hili ni eneo linalomgusa kila mmoja wetu, kuanzia mtu wa kawaida awe mkulima, mvuvi, seremala, mjasiriamali ama yeyote ambaye anahitaji taarifa mbalimbali zimsaidie katika maendeleo yake. Hali kadhalika, mwanafunzi, msomi na mwanataaluma yeyote hawezi kufikia upeo wa masomi na taaluma yake kama hakusoma vitabu na machapisho yaliyoko katika maktaba ambavyo vinatunzwa mkutubi.

Alisema kati ya wilaya 133 zilizopo hapa nchini, ni wilaya 19 tu ambazo zimejenga maktaba katika ngazi ya wilaya. “Hii ni sawa na asilimia 14.2 tu ya wilaya zote. Upungufu huu unasababishwa na tatizo la watu kutotambua umuhimu wa kuwa na maktaba na katika hili lawama ni lazima wabebeshwe Wakurugenzi wa Halmashauri,” alisema. Waziri Mkuu alisema katika ngazi ya mikoa hali si mbaya kwani mikoa 22 kati ya 25 ya Tanzania Bara ina maktaba za mkoa.

“Tunazo Halmashauri 167 lakini ni Halmashauri 19 tu ambazo zina maktaba... nitoe wito kwa wilaya zote ambazo hazina maktaba zione umuhimu wa kuwa na maktaba zake. Tukifanikiwa kuwa na maktaba katika kila mkoa na kila wilaya itatuwia rahisi kuisogeza huduma hiyo katika ngazi ya kata ili iwe karibu zaidi na wananchi,” alisema.

Akisisitiza umuhimu wa fani hiyo Waziri Mkuu alisema mahitaji ya wakutubi hapa nchini ni makubwa kwani hapa nchini kuna shule za msingi zaidi ya 16,300 na shule za sekondari zaidi ya 4,500 za Serikali na za binafsi.

“Tunawahitaji zaidi hawa wakutubi katika shule zetu kwani wakiwepo kwenye shule zetu watakuwa karibu na wanafunzi na wataweza kuwasaidia wanafunzi kupanua uelewa wao,” alisisitiza. Aliahidi kufuatilia maombi ya bajeti ya maendeleo ya chuo ili kukisaidia chuo hicho kiwe bora zaidi.

Mapema akitoa taarifa ya chuo hicho, Mkuu wa Chuo hicho, Bw. Zuberi Khatibu alisema chuo hicho kinakabiliwa na changamoto ya uhaba wa madarasa licha ya kuwa udahili umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

“Mwaka 2007/2008 chuo kilidahili wanafunzi 100 lakini katika mwaka 2012/2013 tulidahili wanafunzi 708 na mwaka huu wa masomo (2013/2014) tumedahili wanafunzi 821,” alisema.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Dk. Alli Mcharazo, alisema kabla chuo hicho hakijaanzishwa hapa nchini, wanafunzi waliokuwa wakitaka kusomea masomo ya ukutubi na uhifadhi nyaraka walilazimika kwenda Makerere, Uganda.

Alisema mbali ya uwepo wa chuo hicho, changamoto kubwa inayowakabili ni ufinyu wa bajeti, uhaba wa miundombinu hasa upungufu wa mabweni na madarasa kiasi kwamba wanalazimika kuwa na shift mbili za masomo (asubuhi na jioni) hali ambayo inaathiri utoaji wa elimu chuoni hapo.

Katika risala yao, wanafunzi wanaohitimu waliomba wapatiwe ajira za moja kwa moja kama ilivyo kwa walimu au askari, pia waliomba maktaba ya chuo hicho ipanuliwe kwa sababu ni ndogo na ikiwezekana chuo kiongezewe kompyuta kwa sababu zilizopo hazitoshi wanafunzi wote kufanya mazoezi kwa vitendo.








All the contents on this site are copyrighted ©.