Kardinali William Levada, Mwenyekiti mstaafu wa Baraza la Kipapa la Mafundisho tanzu
ya Kanisa anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendeleza ari na mwamko
wa maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Benedikto
wa kumi na sita, kwani kila Mwaka unapaswa kuwa ni mwaka wa imani, “hakuna kulala
hadi kieleweke”!
Anapenda kuchukua
fursa hii kwa namna ya pekee kumshukuru Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita kwa kuwa na mwono mpana katika mikakati ya kichungaji, uliolihamasisha Kanisa
kwa kupitia tena nyaraka za Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na kukazia
tena Katekisi makini na endelevu kama sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 20 tangu Mwenyeheri
Yohane Paulo wa Pili alipoichapa kwa mara ya kwanza.
Kardinali Levada anasema
kwamba, cheche za Maadhimisho ya Mwaka wa Imani ambao kwa sasa unaelekea ukingoni
unapata chimbuko lake katika tafakari za wafanyakazi wa Baraza la Kipapa la Mafundisho
tanzu ya Kanisa, walipoona umuhimu wa kufanya tena rejea ya kina kuhusu Mafundisho
ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican na miaka 20 ya Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki,
matunda na changamoto ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Baba Mtakatifu
mstaafu Benedikto wa kumi na sita, akashirikishwa wazo hili, akalikubali na kuridhia
kuitisha Mwaka wa Imani. Maandalizi yakaanza mara moja, kwa kuchapisha mwongozo wa
kichungaji kwa ajili ya Maadhimisho ya Mwaka wa Imani na baadaye Baba Mtakatifu mstaafu
Benedikto wa kumi na sita, akachapisha Waraka wa kichungaji, “Porta Fidei”
Mlango wa Imani.
Kardinali Levada anabainisha kwamba, kuna uhusiano mkubwa
kati ya Uinjilishaji, Katekesi na Mwaka wa Imani. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto
wa kumi na sita, anabainisha mambo makuu mawili katika Maadhimisho ya Mwaka wa Imani
kwamba, utume wa Kanisa unafumbatwa katika Katekesi makini na endelevu pamoja na Uinjilishaji,
mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga na kuimarisha uhusiano wao na Kristo,
kwa kumpenda na kuwaonjesha jirani zao upendo na huruma inayobubujika katika imani
yao kwa Kristo na Kanisa lake.
Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuhakikisha
kwamba, wanashiriki kikamilifu katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu, utume ambao umetekelezwa
na umati wa wamissionari kutoka sehemu mbali mbali za dunia, waliothubutu kujitosa
kimasomaso kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Wamissionari hawa wakakumbana na vizingiti,
changamoto na kinzani, lakini kamwe hawakukata tama na leo hii Kanisa limeenea sehemu
mbali mbali za dunia.
Papa Paulo wa sita, aliwahi kusema kwamba, Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican uliochapisha nyaraka kumi na sita ni Katekesi ya kina na endelevu
kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo, changamoto na mwaliko kwa Mama Kanisa
kusoma alama za nyakati, ili kujibu kwa uhakika kilio na hamu ya mioyo ya watu katika
mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo, ili Injili ya Kristo iendelee kuwa na
mguso na mashiko katika maisha na vipaumbele vya watu.
Mababa wa Mtaguso mkuu
wa Pili wa Vatican walipania kufanya mabadiliko makubwa kwa kuleta hewa safi katika
maisha na utume wa Kanisa; kwa kubadilisha mifumo iliyokuwa imepitwa na wakati. Katekisimu
Mpya ya Kanisa Katoliki ni mchango wa pekee kabisa uliotolewa na Mwenyeheri Yohane
Paulo wa Pili, tangu Maadhimisho ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.
Kardinali
levada anasema, Waraka wa kichungaji wa Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na
sita, Mlango wa Imani una utajiri mkubwa katika hija ya maisha ya kiroho na rejea
kwa waamini katika maisha yao ya kila siku. Ni mlango unaowaowafungulia waamini mahusiano
ya dhati na Mwenyezi Mungu kwa kusikiliza Neno la Mungu linalotangazwa na kuadhimishwa,
tayari kumwilishwa katika uhalisia wa maisha.
Sakramenti ya Ubatizo ni cheti
cha utambulisho wa Mkristo kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, inayomwingiza
mwamini katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Hapa mwamini
anapata fursa ya kujenga na kuimarisha Familia ya Mungu inayotumwa kutangaza na kujenga
Ufalme wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji. Fumbo la Pasaka, liliwasukuma
Wamissionari wengi kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.
Fumbo la Pasaka ni zawadi inayowajibisha na kuendelea kuwachangamotisha waamini kutolea
ushuhuda wa imani tendaji katika medani mbali mbali za maisha.
Kardinali Levada
anabainisha kwamba, kumong’onyoka kwa tunu msingi za: imani, maadili na utu wema ni
kati ya mambo yaliyopelekea kuitishwa kwa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, ili kuangalia
jinsi ambavyo Kanisa linaweza kusaidia kumwilisha Habari Njema ya Wokovu kwa watu
wa nyakati hizi. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitaka kuhakikisha kwamba,
mafundisho tanzu ya Kanisa yanalindwa na kufundishwa kwa ufasaha, kwani ni mafundisho
yanayomkumbatia mtu mzima: kiroho na kimwili.
Nyaraka za Mtaguso mkuu wa Pili
wa Vatican bado ni Katekesi endelevu kwa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu
mamboleo pia ni chachu ya mageuzi ndani ya Kanisa.
Usikose kujiunga nasi tena,
tutakapoendelea kukujuza kwa muhtasari tu: kuhusu Mlango wa Imani na Katekisimu Mpya
ya Kanisa Katoliki. Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. Idhaa ya Kiswahili ya
Radio Vatican.