Utume wa Bahari wachangia dolla za Kimarekani 10,000 kwa ajili ya wahanga wa majanga
nchini Ufilippini
Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na watu wasiokuwa
na makazi maalum, linawashukuru waamini na watu wenye mapenzi mema, ambao wanaendelea
kuchangia kwa hali na mali katika kuokoa maisha ya watu wengi wanaoteseka nchini Ufilippini
kutokana na kukumbwa na tufani ya Haiyan ambayo imesababisha maafa makubwa kwa watu
na mali zao. watu wengi wamepoteza maisha na mamillioni ya watu hadi sasa hayana makazi
ya kudumu.
Baraza la Kipapa kwa namna ya pekee, linapenda kuwakumbuka mabaharia
ambao wako kazini na hawana habari kuhusu hatima ya ndugu, jamaa na marafiki zao nchini
Ufilippini. Wanawashukuru wote wanaowawezesha mabaharia hawa kuwasiliana na ndugu
zao kwa njia ya simu pamoja na kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kielelezo cha
mshikamano wa kiroho na waathirika nchini Ufilippini.
Kitengo cha Utume wa
Bahari kutoka Baraza la Kipapa la shughuli za kichungaji kwa ajili ya wahamiaji na
watu wasiokuwa na makazi maalum, linachangia kiasi cha dolla za Kimarekani 10, 000
kusaidia juhudi za ujenzi mpya wa Ufilippini kwa kushirikiana na idara za utume wa
Bahari nchini Ufilippini, ili kuwawezesha wananchi kuanza tena maisha yao ya kawaida
licha ya magumu wanayokabiliana nayo!