Tamko la hija na kongamano la Mwaka wa Imani toka kwa Familia ya Mungu nchini Tanzania
Maadhimisho ya Mwaka wa Imani nchini Tanzania yamefikia kilele chake hapo tarehe 10
Novemba 2013 kwenye Parokia ya Bagamoyo, Jimbo Katoliki Morogoro, mahali ambapo ni
Mlango na Mwanga wa Matumaini ya Kanisa Katoliki Tanzania. Kilele cha Maadhimisho
ya Mwaka wa Imani, kilitanguliwa na Kongamano la Siku mbili kwa ajili ya Familia ya
Mungu nchini Tanzania. Lifuatalo ni tamko rasmi la hija na kongamano la Mwaka wa Imani
lililotolewa na Askofu Tarcisius Ngalalekumtwa, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki
Tanzania.
1.0 UTANGULIZI Mwaka 2012, Baba Mtakatifu Benedikto wa XVI alitangaza
rasmi Mwaka wa IMANI. Kutokana na Tamko hilo, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania
(TEC), liliazimia kufanya shughuli mbalimbali ili kuchochea IMANI ya Waamini inayokabiliwa
na changamoto zinazoelekea kutawala zaidi katika nyakati zetu na kuathiri IMANI kwa
ujumla.
Ili kutekeleza azma hiyo, Baraza liliagiza kuwe na shughuli mbalimbali
zinazolenga kuchochea IMANI miongoni mwa waamini katika ngazi mbalimbali: JNNK, Parokia,
Jimbo na Kitaifa. Katika ngazi zote hizi kumekuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo hija,
semina, makongamano, na mafunzo mbalimbali yaliyowalenga maaskofu, mapadri, watawa
wa kike na kiume, watoto, vijana, walei na waamini kwa ujumla.
2.0 LENGO LA
MAADHIMISHO YA MWAKA WA IMANI. Lengo la maadhimisho ya mwaka wa IMANI ni kutekeleza
wito wa Baba Mt. Benedikto wa XVI unaohimiza uinjilishaji mpya kwa ajili ya kueneza
IMANI ya Kikristo. Hii ikiwa ni fursa kamili ya kuliingiza Kanisa zima katika kipindi
cha tafakari na ugunduzi wa IMANI ili kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiimani.
3.0 CHANGAMOTO ZA KIIMANI Baadhi ya changamoto za kiimani ni kama zifuatazo: Wakristo
kutawaliwa na malimwengu Mabadiliko makubwa na ya haraka yanayofanya wakristo wazue
au wapaswe kukabili maswali mengi kuhusu maisha na IMANI yetu. Uadui na upinzani
unaojitokeza katika nyanja mabalimbali dhidi ya IMANI na maadili ya Kikristo Kiu
na njaa ya watu wa zama hizi ya kutaka kukutana na Kristo na kufungamana naye. Uhitaji
wa ushuhuda thabiti wa IMANI ya Kikristo.
4.0 HIJA NA KONGAMANO LA
KITAIFA LA MAADHIMISHO YA KILELE CHA MWAKA WA IMANI. Kongamano la Kitaifa la maadhimisho
ya kilele cha mwaka wa IMANI limefanyika tarehe 8 - 10/11/2013 katika Kituo cha Hija
cha Kitaifa, Bagamoyo, Jimbo Katoliki la Morogoro. Jumla ya washiriki wa kongamano
hili ni waamini 1,131 wakiwemo Wahashamu Maaskofu 28, Abate 2, Mapadri 79, Watawa
wasio makleri 183, Walei 310, Vijana 244 na Watoto 285.
Wakati wa maadhimisho
haya, shughuli mbalimbali zimefanyika ikiwemo: Misa Takatifu, Uwasilishaji
wa mada mbalimbali, Kupanda mti wa IMANI kwa kila Jimbo, Kuzindua mnara wa kumbukumbu
wa mwaka wa IMANI Kitaifa, Hija ya Mwaka wa Imani, Burudani
Mada
mbalimbali ziliwasilishwa na kujadiliwa katika vikundi vifuatavyo: Makleri, watawa
wasio Makleri, walei, vijana na watoto. Yafuatayo ni maazimio/tamko la Hija na Kongamano
la kilele cha mwaka wa IMANI:
4.1 Makleri: Kujenga uwezo wa
makatekista na waalimu wa kujitolea ili waweze kutoa mafundisho ya Dini kwa makundi
mbalimbali zikiwemo shule za msingi, sekondari na vyuo. Kuweka mikakati ya kuwajenga
kiimani viongozi wakatoliki wa serikali na siasa ikiwemo kuanzisha “chaplaincy” bungeni
Dodoma. Makleri kuwa karibu na waamini ili kuwasindikiza katika malengo yao ya
kuishi Injili katika ulimwengu. Ekaristi ibaki kiini cha imani yetu.
4.2 WALEI Utengenezwe utaratibu mzuri wa malezi utakaowawezesha mapadri wapya kutekeleza
wito wao kikamilifu. Kuweka msisitizo katika uanzishwaji wa shule za sekondari
za wasichana na kuhakiksha wanapata maandalizi mazuri ya kuwa walezi wa familia. Katiba
ya Halmashauri Walei iruhusu makundi yote ya Walei kushiriki kikamilifu katika kutoa
maamuzi. Kutoa elimu na mafunzo kwa walei na makleri ili kujua majukumu na mipaka
yao. Kuendelea kupata makongamano ya IMANI hasa vijijini. Kuweka shuhuda za
matukio mbalimbali ya kiimani katika Kanisa Katoliki na kuona uwezekano wa kushughulikia
mchakato wa kuwatangaza watakatifu wale waliotuletea Imani Katoliki. Kuweka utaratibu
wa kupeana uzoefu Majimbo kati ya kwa Makleri. Kuwe na mkakati wa kuhuisha JNNK
na ushiriki wa wanaume katika jumuiya. Kuhamasisha walei kugombea nafasi za uongozi
wa kijamii kisiasa na serikali. Kitabu cha mafundisho ya Kanisa kuhusu jamii kichapishwe
na kusambazwa. Tutumie Pro-life ili kupeleka UFATA maeneo ambayo haujafika. Elimu
ya kukabiliana na athari za utandawazi itolewe kwa vijana.
4.3 WATOTO Kuwashawishi
watoto wenzao kuingia kwenye Shirika ili watoto wamjue Yesu. Kuwa na upendo kwa
watoto wenzao hasa wale wenye matatizo ili wadumu katika umisionari Kusaidia maskini
na wagonjwa na pia kuwa na siku moja ya kutembelea yatima (watoto) wagonjwa n.k. Kutoa
mrejesho wa kongamano kwa watoto wenzao kwa yale waliyoyapata. Wazazi wasiwakataze,
bali wahamasishe watoto kuingia kwenye Utoto Mtakatifu. Watoto wafundishwe dini
vizuri.
4.4 WATAWA Kutoa malezi endelevu kwa Watawa wote ili
kuwaimarisha kiimani, kimaendeleo na kimtandao (mawasiliano) Kutoa huduma ya
masakramenti na nafasi ya kuwasikiliza watu Watawa wapatiwe mahitaji muhimu, ikiwemo
elimu, kutokanana na utume wao Parokiani/Taasisi za Jimbo n.k ili kuboresha utume
kuendana na karama za shirika. Wakuu wa mashirika watume watawa wao katika utume
kadiri ya uwezo. Mashirika ya kitawa yawe na mikataba na jimbo ili kuboresha utekelezaji
wa utume kidini kuendana na karama za shirika na mazingira ya jimbo (inapowezekana
kuwe na hati miliki za ardhi, mashamba n.k). Maparokiani mashirika ya kitawa na
mapadre tuwe na utume pamoja ili kufanikisha kazi ya ufundishaji dini. Tuwe na vitendea
kazi n.k. Tunahitaji kuimarisha Watawa katika kutoa huduma hasa huko Zanzibar ambapo
ukristo unapingwa.
4.5 VIJANA: Kanisa litumie wataalamu wake
wenye taaluma zao ili kupunguza gharama zake. Kanisa lazima litafute vitega uchumi
vingine badala ya kutegemea sadaka na zaka pekee ili kutegemeza Kanisa. Kuwe na
mafundisho endelevu baada ya Ekaristi Takatifu, kipaimara na ndoa kwa vijana.
HITIMISHO Hija
na Kongamano hili la Mwaka wa IMANI limetoa fursa ya kutimiza mwaliko wa Baba Benedikto
wa XVI wa kujitathmini KIIMANI kama muumini mmoja mmoja na kama Kanisa linalosafiri.
Limetoa mwelekeo wa tulikotoka, tulipo na tunapopaswa kuelekea katika IMANI yetu ya
kikristo na hasa katika kukabiliana na changamoto zetu za sasa.
Ndugu zangu
waamini wanafamilia ya Mungu, mwisho wa hija na kongamano hili ni mwanzo wa utekelezaji
wa maazimio tuliyofikia leo ili tuwe chumvi yenye ladha na mwanga katika kukoleza
maisha ya binadamu wa leo waweze kuonja matunda ya IMANI yetu.
Kwanza kabisa
tunamshukuru Mwenyezi Mungu aliyetupa nafasi hii ya kuweza kuitafakari imani yetu.
Pili
tunawashukuru waamini wote, walioshiriki kwa hali na mali, katika kufanikisha kongamano
hili wakiwemo:- Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na Wahashamu
Maaskofu wote. Kamati mbalimbali za kongamano. Wakuu wa Mashirika ya Kitawa,
ya kike na kiume. Taasisi mbalimbali za Kanisa vikiwemo Vyuo Vikuu na Seminari. Waamini
wote. Jimbo Katoliki la Morogoro na namna ya pekee Mapadri wa Shirika la Roho Mtakatifu. Taasisi
za Serikari na vyombo vya Usalama. Vyombo vya Habari na Wanakwaya. Wadau wote
walioshiriki kwa namna mbalimbali wakiwemo wenye Mahoteli, vyombo vya Usafiri pamoja
na Uongozi na wafanyakazi wote wa Stella Maris wakiwemo wapishi.
+
Tarcisius J.M. Ngalalekumtwa RAIS WA TEC/ASKOFU JIMBO LA IRINGA