Simameni kidete kupinga utamaduni wa kifo, kumbatieni matumaini ya zawadi ya maisha!
Waamini, watu wenye mapenzi mema, vyama vya kitume na kiraia, Jumapili tarehe 17 Novemba
2013 vinafanya maandamano makubwa nchini Hispania kupinga tabia ya baadhi ya viongozi
kukumbatia sera na utamaduni wa kifo! Wanapenda kutoa mwaliko wa kusitisha sera za
utoaji mimba na kuanza mchakato wa matumaini yanayokumbatia zawadi ya uhai kutoka
kwa Mwenyezi Mungu.
Haya ni maandamano ya nne kufanyika nchini Hispania katika
harakati za kupinga utamaduni wa kifo.
Maandamano haya ni kielelezo cha sauti
ya Familia ya Mungu nchini Hispania kuiomba Serikali yao kusimama kidete kulinda na
kutetea zawadi ya uhai, kama walivyoahidi wakati wa kampeni ya kutaka kuingia madarakani,
lakini inaonekana kwamba, mara tu baada ya kuingia madarakani, wamesahau ahadi yao
na kuanza kukumbatia utamaduni wa kifo, kwa kupitisha sera na sheria zinazohalalisha
utoaji mimba nchini Hispania. Waamini na watu wenye mapenzi mema wanasema, utoaji
mimba uwe zero! watu wajenge utamaduni wa kuenzi zawadi ya uhai bila masharti!