Wakristo na Waislam wajitaabishe kufahamiana ili kujenga misingi ya haki, amani na
utulivu kwa ajili ya mafao ya wengi!
Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria anawaalika
Wakristo na Waislam kujenga utamaduni wa majadiliano ya kidini, kwa kujibidisha kufahamiana
kwa dhati, ili kujenga misingi ya haki, amani na utulivu, wote kwa pamoja wakipania
kutafuta mafao ya wengi. Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na utamadunisho, ili
kweli za Kiinjili ziweze kuingia katika maisha na vipaumbele vya waamini, ili Mkristo
aweze kuwa kweli Mkristo na hapo hapo akiendelea kuwa ni Mwafrika pasi na mawaa!
Askofu
mkuu Kaigama ameyasema hayo hivi karibuni wakati wa Maadhimisho ya Sinodi ya tatu
ya Jimbo Katoliki la Enugu, nchini Nigeria. Haki msingi, utu na heshima ya binadamu
ni mambo muhimu yanayopaswa kuwa msingi wa majadiliano ya kidini na kamwe watu wasikubali
kugawanywa kwa misingi ya ukabila na udini.
Jamii za Kiafrika zijifunze kuenzi
mila, desturi na tamaduni nzuri zinazopatikana kutoka katika makabila mbali mbali.
Kwa Mwafrika wa kweli: ukarimu, upendo kwa maisha ya Kijumuiya, heshima kwa wazee
ni mambo yanayopewa kipaumbele cha pekee. Mambo haya yakizingatiwa miongoni mwa Waafrika,
kinzani, chuki, vita na uhasama wa kidini vitatoweka kama umande wa asubuhi.
Ingawa
Nigeria ni kati ya nchi ambazo zinakabiliwa na tatizo la ukabila na udini, Askofu
mkuu Kaigama anasema, bado wananchi wa Nigeria wanaweza kujikita katika mchakato wa
majadiliano ya kidini na kiekuemene kwa ajili ya ustawi na mendeleo ya wengi; haki
na amani. Ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana, rushwa na ufisadi ni kati
ya mambo ambayo yanawaandama wananchi lakini, wajanja wachache wanatumia migogoro
ya kidini kwa ajili ya kukwepa uwajibikaji.
Licha ya majanga yanayoendelea
kusababishwa na kikundi cha kigaidi cha Boko Haram, lakini bado Waislam na Wakristo
wanaendelea kushirikiana kwa mambo mengi na kwamba, watu wachache wasiruhusiwe kuvuruga
amani, utulivu na kiwango cha maendeleo kilichofikiwa!