2013-11-15 07:23:35

Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa


Tunaendelea kama kawaida katika kipindi chetu, tafakari masomo Dominika, na leo tunatafakari masomo Dominika ya 33 ya mwaka C wa Kanisa. RealAudioMP3

Tayari tunaelekea kumaliza mwaka wa Kanisa, yaani tukiijongea Dominika ijayo iliyo Dominika ya mwisho ambapo tutasherehekea Sikukuu ya Yesu Kristo Mfalme wa ulimwengu. Masomo yote matatu yanachukua sehemu ya tafakari juu ya mwisho wa dunia, ambayo hasa ndiyo tabia ya Dominika zote za mwisho wa mwaka wa Kanisa. Tabia hii kwa kifupi twaiona katika somo la pili ambapo inaonekana katika jumuiya ya kwanza ya kikristu na hasa kati ya Wakristo wa Thesalonike watu walianza kuacha kufanya kazi wakitarajia ujio wa pili wa Bwana kuwa karibu.

Katika hilo Mtakatifu Paulo anawaonya akiwaambia yakuwa yampasa kila mmoja kufanya kazi, uvivu unaojilaza katika subira ya ujio wa Bwana haukubariki. Katika hili tunaweza kuona pia thamani ya kazi katika maisha ya mwanadamu. Kazi iwayo yote iwe ya mikono au ya kiakili au ya kiroho ni ya maana mbele ya Mungu, aliyesema mkaitiishe nchi.

Mpendwa msikilizaji, kama nilivyokwisha dokeza yakuwa masomo yetu, yatupa hali itakavyokuwa wakati wa mapambazuko ya uzima wa milele, tunakutana na hali hiyo katika lugha inayotisha na pengine yaweza kumfanya mtu aogope, na hasa katika ile hali ya kutarajia maneno ya faraja na huruma. Hata hivyo hali hii ya kutisha ina maana yake na baadaye itawekwa sawa na Mungu mwenyewe. Tunajua hilo kwa sababu kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu hata kama ni zito na kali lakini huwekewa mafuta na kugeuka kuwa Neno na tangazo la matumaini kwa mpokeaji aliyeshiba imani!

Mpendwa msikilizaji, kwa sababu hiyo basi yafaa kutenganisha kati ya maneno au lugha itumikayo na ujumbe ambao Mungu apenda kutupatia. Lugha inayojitokeza katika masomo ya Dominika za mwisho za mwaka ni lugha ya kiufunuo, lugha ambayo tunakutana nayo daima katika kitabu cha Ufunuo. Ni wa namna hiyo basi kila mmoja wetu awe makini katika kupembua ujumbe wa Neno la Mungu, asije akaangukia katika shimo la upotoshaji wa Habari Njema.

Mpendwa msikilizaji, tunasema hili kwa sababu ulimwengu wa leo ambao umejaa fitina, ujangili pamoja na ughaidi unaweza kumfanya mtu badala ya kujenga matumaini na kusonga mbele katika kutafuta amani, basi akaona hakuna haja kwa maana ni mikasa tu ndiyo inayotuzunguka! Kuna baadhi ya wenzetu ambao pasipo kutafakari na kuchekesha vema huibuka na mahubiri vitisho kuhusu mwisho wa dunia na huwajengea watu imani ogopeshi ambayo haizaliwi toka upendo wa Kristu msalabani bali katika vionjo vya watu, imani inayosisitiza hukumu badala ya upendo wa Mungu kwa wanadamu.

Mpendwa mwana wa Mungu, tazama upendo wa Mungu pale msalabani, u-wazi anapomwambia yule mwizi tangu leo utakuwa pamoja nami mbinguni! Bwana hapendi tumwogope bali tumpende, kwa maana hakuna atakayepatilizwa kumbuka anasema “walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu! Inatosha tu pasipo kuogopa kusubiri na katika subira hiyo basi tutaziponyesha nafsi zetu. Upendo wa Mungu haurudi nyuma, jicho alilomtazama Zakayo ndilo hilohilo jicho la milele ambalo atatutazama nasi katika nyakati za mwisho na sasa. Katika hii basi Mungu anatudai kutumaini daima kama ambavyo yeye ni tumaini la kweli.

Kwa nini jambo hili? Jambo hili linakuja katika tafakari kwa maana katika maisha yetu kuna kishawishi kikubwa cha kuacha njia ya Bwana, njia nyembamba, njia ya maisha na kufuata njia pana, njia ya kupoteza, njia ya kifo wakati wa taabu na shida katika maisha yetu ya kila siku. Kumbukeni daima njia ya wokovu ni ndefu, ni siri ya Mungu ambayo hufunuliwa kwa kila mmoja wetu katika tumaini la kweli. Ndiyo kusema nabii Malaki anasema kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia lenye kuponya katika mbawa zake. Kumbe siri ya Mungu tunaigundua katika kulicha jina lake na kutumaini wokovu pasipo kusita.

Mpendwa mwana wa Mungu, wanaolicha jina la Mungu ni wale ambao kila siku ya maisha yao hutekeleza nyajibu zao katika familia na mahali pa kazi kwa upendo usiodai faida bali unaolala na kujisimika katika matumaini na upole wa moyo. Katika kujenga tumaini basi ni rahisi yatakapojitokeza matukio ya kutisha tunayoyasikia katika Injili, mwamini kusima na kusonga mbele katika subira pasipo woga na kulicha jina la Bwana.

Hili lina maana ya kwamba tusihangaike kutafuta namna ya ajabu ya kuishi ukristu wetu bali namna ya kawaida iliyojaa mapendo thamini kwa ndugu na jirani kama alivyofanya Msamaria mwema. Tukitenda kile cha kawaida kama Mtakatifu Thereza wa Mtoto Yesu, basi tutakuwa na uhakika wa kujipatia njia nyembamba hata katika mateso tunayokumbana nayo kila siku ya maisha yetu.

Basi mpendwa, tunapoelekea kufunga mwaka wa Kanisa tunaalikwa kuwa na kitu cha kuweka mbele ya Mungu kama tiketi yetu ya kuonana naye, na hivi basi usisahau kabisa yakwamba tumaini lako na imani yako tendaji inayojenga familia ya Mungu ndizo tiketi mwafaka kwa ajili ya sherehe hiyo.

Mpendwa msikilizaji, Baba Mtakatifu Francisko katika barua yake ya Kitume Mwanga wa Imani , anatufundisha kuwa mwanga wa imani unadai kuwekwa katika huduma ya sheria ya haki, na amani, mwanga huo unakuwa ni uwezo unaoongeza nguvu katika mahusiano ya binadamu, na katika kuboresha maisha ya pamoja na mshikamano wa kijamii. Imani inafanya sisi kufahamu usanifu wa mahusiano kati ya binadamu kwa sababu imani huzingatia msingi ya adilifu katika muono wa sheria za Mungu. Na hivyo imani inakuwa huduma kwa manufaa ya wote.


Mpendwa, imani ni zawadi ambayo inadai kutunzwa pia ili isipotee na haipaswi pia kutunzwa tu katika moyo wetu bali lazima ijitokeze nje ili kuweza kushirikisha wengine tumaini la kweli na upendo wa Mungu kwa ajili ya wote. Imani huimarisha wengine na hivi tukaweza sote kuwa tayari kuisubiria siku ya mwisho kwa furaha.

Nikutakie furaha na tumaini la kweli katika Mungu Mkuu, mpaji wa mapaji na zawadi zote za mbinguni. Tumsifu Yesu Kristo.
Tafakari hii imeletwa kwako na Pd Richard Tiganya, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.