2013-11-15 11:42:35

Familia inapaswa kupewa kipaumbele cha pekee katika sera na mikakati ya nchi!


Baba Mtakatifu Francisko wakati wa ziara yake ya kikazi kwenye Ikulu ya Italia, Alhamisi, tarehe 14 Novemba 2013, amemshukuru Rais Giorgio Napolitano kwa kumpatia nafasi ya kuweza kukutana na kuzungumza na wafanyakazi wa Ikulu ya Italia pamoja na familia zao. Amewataka wafanyakazi hao kuonesha moyo wa upendo na mshikamano pamoja na jirani zao katika medani mbali mbali za maisha.

Amewapongeza kwa kazi kubwa wanayoufanya hata wakati mwingine bila ya kuonekana na wengi, lakini muhimu kwa ustawi na maendeleo ya taifa la Italia. Baadhi yao ni wale wanaokumbana uso kwa uso na majanga ya maisha katika ngazi ya kijamii, familia na mtu binafsi yanayowasilishwa kwa Rais kwa ajili ya maamuzi na utekelezaji wake. Amewataka wafanyakazi wa Ikulu ya Italia kujenga na kudumisha moyo wa ukarimu na uelewa kwa wote wanaokutana nao!

Jamii inawahitaji watu wanaojisadakisha kwa weledi, utu na uelewa wa kibinadamu, daima wakionesha moyo wa mshikamano hasa kwa wanyonge na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Baba Mtakatifu mwishoni, anawataka wafanyakazi wa Ikulu kutoka tamaa wanapokumbana na vizingiti katika maisha na utekelezaji wa majukumu yao, bali wawe tayari kusaidiana na kutiana moyo, ili kwa pamoja waweze kusonga mbele kwa matumaini zaidi.

Baba Mtakatifu amewahakikishia sala zake na amewaomba kuendelea kumwombea katika maisha na utume wake, kwani anahitaji zaidi sala za kila mmoja wao!







All the contents on this site are copyrighted ©.