2013-11-14 09:19:07

Mwaka wa Imani Jimboni Singida ulilenga kuimarisha utume na maisha ya Makatekista!


Katika kutekeleza tamko la Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI, kuwa mwaka 2013 ni mwaka wa Imani, Jimbo Katoliki Singida pamoja na majimbo yote Tanzania walipokea mwito huo kwa hamasa kubwa kwa nia ya kuhuisha imani kwa vitendo.

Maswali yakilenga kwenye misingi yetu ya imani ili kuona kweli kama bado tumesimama imara au tunayumbayumba hasa kutokana na kushambuliwa kwa imani, kukithiri kwa utandawazi, imani kuonekana kama kitu binafsi, kutaka kumwondoa Mungu katikati ya matukio yetu ya maisha na maisha kwa ujumla nk. Kutafakari maadui wakubwa wa imani na jinsi ya kukabiliana nao, kuhuisha maisha ya Kikristo kwa kuyasoma tena na tena Maandiko Matakatifu, Nyaraka za Mtaguso Mkuu wa pili wa Vatican, na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki. Haya yote yakiwa ni rejea katika kuuishi Mwaka wa Imani.

Mbali na kuadhimisha mwaka wa imani, Jimbo Katoliki Singida liliuita mwaka huu kuwa ni mwaka wa Makatekista. Hii inatokana na ukweli kwamba, Makatekista ni wasaidizi wakubwa wa mapadre katika kufundisha imani. Hivyo ukawekwa mkakati wa kutambua utume wao katika jumuiya za waamini, yaani kuanzia ngazi za Jumuiya, Vigango, Parokia na Jimbo.

Ili kuitikia wito huo kiparokia, Maparoko wa Parokia za Chibumagwa (Pd. Mulokozi Deusdedit, C.PP.S) na Kintinku (Pd. Moses Gwao) wakishirikiana na kamati tendaji na Halmashauri ya Walei wa parokia hizo waliona ni vyema kufungua na kufunga mwaka huo kwa pamoja kama kuonesha ujirani mwema kiimani.

Hivyo, tarehe 10/2/2013 Misa kubwa ya ufunguzi ilifanyika katika Parokia ya Bikira Maria Mpalizwa-Chibumagwa ambapo waamini wa parokia zote mbili walishiriki kwa kishindo kikubwa. Katika ibada hiyo Makatekista walirudia kiapo chao cha uaminifu katika kufundisha imani ya kweli na kuendelea kuwa waaminifu katika uongozi wa Kanisa. Walirudia ahadi zao kwa kusali Kanuni ya Imani wakiwa na mishumaa inayowaka kama ishara ya uwepo wa Kristo shahidi mkuu na mwanzilishi wa imani yao. Vile vile watoto wapatao sita walibatizwa. Misa hiyo iliongozwa na Pd. Mulokozi Deusdedit, akishirikiana na Mapadre watanao na Mashemasi wawili.

Sasa, Parokia hizi mbili tayari wameanza mchakato wa kufunga mwaka wa imani, kama walivyofungua pamoja wamekubaliana kwenye kikao kuwa Misa ya kufunga itafanyika katika Parokia ya Kintinku tarehe 30/11/2013. Ibada takatifu ya misa itaanza saa 3:00 asubuhi ikitanguliwa na maandamano yatakayoanza saa 1:45 asubuhi. Mbali na mambo mengine dhamira kuu ni kuwaenzi Makatekista ambao wamekuwa msitari wa mbele katika: kuikiri, kuifundisha, kuiishi kwa vitendo sanjari na kuisali katika vigango vyao.

Katika ibada hiyo Makatekista 42, watatunukiwa vyeti kama ishara ya kutambua mchango wao katika kuipokea, kuiishi, kuifundisha na kuisali imani. Kati yao wapo Makatekista 3 ambao wameanza utume wao mwaka 1963.

Alama ambazo zimechaguliwa kwenye vyeti vyao ni pamoja na Biblia na Msalaba. Bila kusahau Nembo ya mwaka wa imani kuwa ni mtumbwi ambao wote tumo tukisafiri kwa pamoja kumwelekea muasisi wa imani ambaye ni Kristo mwenyewe. Na kwa kuyakumbuka maneno ya Mtume Paulo "Simameni imara katika imani yenu" (1Cor. 16:13), waamini wote watakumbushwa wajibu walio nao katika kutunza imani ambayo thamani yake ni kubwa katika maisha yao.

Akiwakumbusha umuhimu wa mwaka wa imani Baba Paroko wa Parokia ya Chibumagwa Pd. Mulokozi Deusdedit alisema: mwaka wa imani ni tunu kwetu, kujifunza upya misingi ya mafundisho yetu ya imani, tupokee wongofu mpya na wa kweli. tunaangalia imani kama mwenzi anayetusaidia kutambua maajabu anayotenda Mungu. tunaalikwa kusoma, kutafakari, na kulimega Neno la Mungu, kujiimarisha katika kulijua, ili tubidiishwe na kushibishwa nalo.

Imani yetu itufanye tujibu upendo wa Mungu wa Yeye kujifunua kwetu. Imani itusaidie kujibu swali la Nini maana ya maisha yetu. yaani kumjua, kumpenda, na kumtumikia Mungu na mwisho kufika kwake mbinguni. Shughuli zetu za kuajiriwa katika nafasi mbalimbali maofisini, biashara zetu, mashamba yetu, ufugaji wetu, je, vinatusaidia kujibu swali hilo?

Imani ni kipawa kutoka kwa Mungu, ili kwa neema ya Mungu tupate kufikia wongofu. Neno la Mungu linatakiwa kutupyaisha, kwa kulisikiliza kwa makini na kung'amua kile ambacho Roho Mtakatifu analiambia Kanisa.
Imani itusaidie kutambua thamani ya tunu bora za kibinadamu kama vile: ndoa takatifu, kuthamini maisha na kuachana na utamaduni wa kifo, kuacha kuaharibu mimba, madawa ya kulevya, nk. Imani inawataka watu wawe na matamanio ya matashi halali kama vile kuyakemea kwa jina la Yesu yale yote yanayotaka kuingiza mawazo au matendo ya jinsia moja.

Imani inatudai uwajibikaji kuanzia kwenye familia, jumuiya, makazini, taifa kwa ujumla wake, Kanisa kwa ujumla wake, kama anavyotufundisha Mtakatifu Yakobo kwenye barua yake kwa watu wote. (2:14)"….kuna faida gani mtu kusema ana Imani lakini haoneshi kwa matendo." Tuseme kaka au dada hana nguo, au chakula, yafaa kitu gani kuwaambia hao nendeni salama mkaote moto na kushiba bila kuwapatia mahitaji yao ya maisha? Vivyo hivyo Imani peke yake bila matendo imekufa kwa sababu haitazaa matunda.
MWALIKO
Waamini wote wa Parokia za Kintinku na Chibumagwa pamoja na waamini wote, na watu wenye mapenzi mema wanakaribishwa kwenye misa takatifu tarehe. 30/11/2013 katika parokia ya Kintinku ili kumsifu Mungu na kujivunia imani yetu katika matendo. Imani yetu ni shirikishi. Imani yetu ni hai na ni katika nafsi ya Yesu Kristo. WOTE MNAKARIBISHWA.
Pd. Mulokozi Deusdedit, C.PP.S.
Paroko wa parokia ya Bikira Maria mpalizwa mBinguni - Chibumagwa
Jimbo Katoliki Singida. Tanzania.








All the contents on this site are copyrighted ©.