Mkutano wa mabadiliko ya tabianchi unaendelea mjini Varsavia, Poland
Mkutano wa kumi na tisa kuhusu mabadiliko ya tabianchi utakaodumu kwa siku kumi unaendelea
mjini Varsavia, nchini Poland, kwa kuwajumuisha wajumbe kutoka katika nchi 195 duniani.
Mkutano huu umefunguliwa rasmi hapo tarehe 12 Novemba 2013 na Bwana Abdullah Bin Hamad
Al Attiyah, Waziri mkuu wa zamani wa Qatar. Katika hotuba yake ya ufunguzi amezipongeza
nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa kwa kuridhia itifaki ya Kyoto.
Wajumbe
wanasema, matatizo na changamoto za mabadiliko ya tabianchi ni mwaliko kwa Jumuiya
ya Kimataifa kushikamana kwa pamoja ili kutafuta suluhu ya kudumu, kwani majanga yanayoendelea
kujitokeza sehemu mbali mbali yanaonesha umuhimu wa kushirikiana kwa dhati, ili kuacha
urithi wa kudumu kwa kizazi kijacho.
Mkutano huu unapania pamoja na mambo
mengine kuanzisha mchakato wa itifaki ya kimataifa pamoja na udhibiti wa uzalishaji
wa hewa ya ukaa, katika mkutano kama huu utakayofanyika mjini Lima kunako mwaka 2014
na hatimaye, kutiwa sahihi na nchi wanachama mwaka 2016 mjini Paris, Ufaransa. Lengo
la Umoja wa Mataifa ni kupunguza nguzi joto kwa kiasi cha nyuzi joto mbili, jambo
ambalo bado linaonekana kuwa ni tete!