Askofu mkuu Dominique Mamberti, Katibu mkuu wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano
wa kimataifa mjini Vatican anasema, cheche za kukubali kushiriki katika mchakato wa
kutafuta amani nchini Syria kwa njia za kidiplomasia ni jambo linalotia moyo, hasa
kwa kuzingatia kwamba, machafuko ya kisiasa na vita yameendelea kusababisha maafa
makubwa kwa watu wasiokuwa na hatia.
Majadiliano ndiyo njia pekee inayoweza
kusaidia upatikanaji wa amani ya kuduni nchini Syria. Watu wanaendelea kupoteza maisha
na mali kutokana na vita. Umoja wa wapinzani wa Serikali kitaifa umeridhia uamuzi
wa kushiriki katika majadiliano ya kidiplomasia kimataifa, ili kutafuta suluhu ya
kudumu ya vita inayoendelea nchini Syria. Ujumbe wa Vatican una unga mkono juhudi
hizi pamoja na kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa waathirika wa vita.
Baba
Mtakatifu Francisko anafuatilia kwa ukaribu zaidi mateso na mahangaiko ya wananchi
wa Syria na Mashariki ya Kati kwa ujumla wake, ndiyo maana tarehe 5 Septemba 2013
aliitisha siku maalum kwa ajili ya kusali na kufunga ili kuombea amani nchini Syria.
Wanasiasa wakionesha utashi wa kweli, vita nchini Syria vinaweza kusitishwa na watu
wakaanza maisha ya kawaida anasema Askofu mkuu Mamberti.
Jambo la pili ni
kusitisha biashara ya silaha nchini Syria kwani biashara hii pia ni kichocheo kikubwa
cha machafuko ya kisiasa na kijamii na matokeo yake ni vita na maafa kwa watu wasiokuwa
na hatia. Wananchi wa Syria hawana budi kuanzisha mchakato wa upatanisho, haki na
amani; kwa kukazia umoja na mshikamano wa kitaifa bila ubaguzi na upendeleo kwa misingi
ya kidini.