Mtaalam wa haki msingi za binadamu kutoka Umoja wa Mataifa Najat Maala M'jid, hivi
karibuni ameitaka Serikali ya Benin kuhakikisha kwamba, inasimama kidete kulinda na
kutetea haki msingi za watoto ambazo zinapaswa pia kuwa ni sehemu ya ajenda zake za
kisiasa.
Kuna maelfu ya watoto wanaonyanyaswa na kudhulumiwa na wahusika wa
vitendo hivi vya aibu bado hawajakamatwa ili wafikishwe kwenye mkondo wa sheria. Watoto
wamekuwa wakikamatwa na kutumbukizwa kwenye biashara haramu ya binadamu; wanafanyishwa
kazi ngumu zinazowadumaza: kimwili na kisaikolojia; watoto hao pia wamekuwa ni vivutio
vikubwa vya biashara ya ngono inayoendelea kushamiri nchini Benin, kinyume cha haki
msingi za binadamu, utu na maadili mema.
Taarifa hii ni matokeo ya safari
ya kikazi iliyofanywa na Bibi Najat Maala M'jid nchini Benin hivi karibuni kwa kukutana
na kuzungumza na viongozi wa Serikali, vyama vya kiraia na waathirika wa vitendo hivi
vya kinyama. Wasichana nchini Benin ndio waathirika wakuu wa nyanyaso za kijinsia,
ingawa kuna sheria zinazodhibiti vitendo vya uhalifu dhidi ya wanawake na watoto,
lakini hazitekelezwi na kwamba, kilio na mahangaiko ya watoto nchini Benin hayasikilizwi.
Bibi
Najat Maala M'jid anasema, kuna haja ya kuwa na sera makini zinazolinda maisha, ustawi
na maendeleo ya watoto nchini Benin, dhidi ya watu wachache wanaotaka kujinufaisha
wenyewe kwa njia za nyanyaso na madhulumu. Ili kufanikisha lengo hili kuna haja kwa
Serikali na Jumuiya ya Kimataifa kutenga rasilimali fedha na watu ili kurahisisha
utekelezaji wa mikakati inayopania kulinda watoto dhidi ya nyanyaso na dhuluma.