2013-11-11 10:19:42

"Mnanolewa ili kuendeleza dhamana na utume wa Uinjilishaji kwa Makanisa mahalia"


Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumamosi iliyopita, tarehe 9 Novemba 2013 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya ufunguzi rasmi wa Mwaka wa Masomo kwa Mapadre wanafunzi wanaosoma kwenye Chuo cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, kilichoko mjini Roma sanjari na kubariki bweni lililofanyiwa ukarabati mkubwa tayari kuanza kutumiwa na Mapadre wanafunzi kutoka katika mataifa 42 yanayounda nchi za Kimissionari.

Katika mahubiri yake, Kardinali Filoni amewakumbusha Mapadre wanafunzi kwamba, lengo la Kanisa kuwaleta mjini Roma ili kupata elimu ya juu kwa kuwaaminisha mikononi mwa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, ni kujikita zaidi katika kuendeleza kazi ya Uinjilishaji wa watu kwa ari na kasi kubwa zaidi, kwa kuwapatia elimu bora ili waweze kutekeleza dhamana na utume wao kwa ufanisi na tija.

Kipindi cha masomo kwa miaka miwili au mitatu ni sehemu ya mchakato wa malezi endelevu, jambo muhimu linalokaziwa na Mama Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Ni kipindi cha kujiendeleza katika makuzi ya kiroho, maadili mema na maisha ya Kijumuiya, ili kuonjeshana na kumegeana utajiri wa mila na tamaduni kutoka katika nchi za Kimissionari. Hii ni nafasi adimu inayopaswa kutumiwa kikamilifu na Mapadre wanafunzi wakati wote wanaponolewa hapa mjini Roma.

Kardinali Filoni anasema, Maaskofu na Kanisa kwa ujumla linapenda kuwekeza katika majiundo makini kwa Makleri wake, ili kuendeleza kazi na dhamana ya Uinjilishaji utume ambao Mama Kanisa anatumwa kuuendeleza hadi miisho ya dunia. Mapadre hawa wamekumbushwa kwamba, wameitwa na Mwenyezi Mungu hata bila mastahili yao na kwamba, wote ni sawa na wanapendeka mbele ya Mwenyezi Mungu.

Kardinali Filoni anasema kwamba, Mwenyezi Mungu amewaita na anawajalia faraja watu wake na kuimarishwa kwa nguvu na uwezo wa Roho Mtakatifu, ili kutekeleza dhamana na utume wao ndani ya Kanisa. Anasema, Kanisa lipo na litaendelea kuwapo kwani linahamasishwa na Kristo kwenda kutangaza Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Uinjilishaji ni sehemu muhimu sana ya utume na maisha ya Mama Kanisa, dhamana wanayokabidhiwa pia Mapadre kuiendeleza katika Makanisa yao mahalia.

Takwimu kutoka Chuo Kikuu cha Mtakatifu Petro mjini Roma zinaonesha kwamba, kuna jumla ya Mapadre wanafunzi 166, kati yao kuna Mapadre 97 kutoka Barani Afrika na 69 wanatoka Barani Asia. Kuna jumla ya Mapadre wanafunzi wapya 117 waliofika mjini Roma kuanza mwaka wa masomo 2013- 2014.

Ibada ya misa sanjari na kubariki bweni lililofanyiwa ukarabati mkubwa, imehudhuriwa na Askofu mkuu Savio Hon Tai Fai, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu mwambata na Rais wa Mashirika ya Kimissionari ya Kipapa pamoja na viongozi wengine waandamizi kutoka katika Baraza na Vyuo Vikuu vya Kipapa vilivyoko mjini Roma.

Imeandaliwa na Padre Alfred Kwene,
Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Petro, Roma.







All the contents on this site are copyrighted ©.