Maaskofu wanaangalia vyombo vya mawasiliano ya jamii vinavyoweza kutumika katika Uinjilishaji
wa watu barani Ulaya
Uinjilishaji wa roho za watu Barani Ulaya ni mada ambayo imeongoza mkutano wa siku
tatu wa Maaskofu wenye dhamana na vyombo vya mawasiliano ya jamii kutoka Shirikisho
la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Ulaya, (CCEE). Maaskofu wameangalia kwa kina na mapana
changamoto na vyombo vilivyopo vinavyoweza kutumika kwa ajili ya kutangaza Habari
Njema ya Wokovu kwa Makanisa Barani Ulaya, eneo ambalo linaendelea kupokea idadi kubwa
ya watu kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Mkutano wa Maaskofu umeandaliwa
na kudhaminiwa na Tume ya Mawasiliano ya Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki
Ulaya. Viongozi wakuu wa Kanisa wamepata nafasi ya kuchangia mawazo yao kuhusu changamoto
na nyenzo ambazo zinaweza kutumiwa na Mama Kanisa katika dhamana ya utangazaji wa
Habari Njema ya Wokovu kwa Mataifa Barani Ulaya.
Askofu mkuu Claudio Maria
Celli, Rais wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano ya Jamii alipewa wajibu wa kupitia
kwa ufupi yaliyojiri katika Hati juu ya Mawasiliano iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso
mkuu wa Pili wa Vatican na maendeleo yake katika kipindi cha miaka 50 iliyopita. Amegusia,
historia, mabadiliko na changamoto ambazo zimejitokeza tangu wakati huo. Wajumbe pia
wameangalia namna ambavyo Kanisa linaweza kujitosa kunadi Injili katika soko la kimataifa.
Kardinali Martines Sistach anasema, Maaskofu wameangalia kwa pamoja dhamana
ya kimissionari mintarafu tamaduni za Ulaya sanjari na maendeleo ya sayansi na teknolojia
ya habari kama nyenzo muhimu ya Uinjilishaji. Mitandao ya kijamii ni jukwaa jipya
linaloweza kutumiwa kikamilifu na Mama Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya.
Lakini ni vyombo vinavyohitaji kuwa na mwelekeo mpana zaidi, kwani ni mitandao
inayogusa maeneo maalum ya maisha ya watu. Kanisa lisipokuwa makini, linaweza kujikuta
kwamba, linatenga idadi kubwa ya watu wasiokuwa kwenye mitandao. Kuna haja bado kwa
Mama Kanisa kuhimiza anasema Kardinali Sistach umuhimu wa kufahamiana na kujenga mahusiano
ya dhati ndani ya Jamii husika. Jumuiya zinazoundwa kwenye mitandao ziendelee kuwepo,
lakini pia wale wasioguswa na mitandao ya kijamii, wasaidiwe kikamilifu kuona utamu
wa Injili.
Ili Kanisa liweze kutekeleza barabara dhamana ya Uinjilishaji kwa
njia ya mitandao ya kijamii, kuna haja ya kuwaandaa wataalam watakaotekeleza dhamana
hii nyeti; kwa kutenga: rasilimali, muda na nguvu zao, ili kuwawezesha watu hao kujisikia
kuwa kweli ni sehemu ya Jumuiya ya Kanisa, inayojitahidi kumwilisha Ujumbe wa Injili
katika uhalisia wa maisha yao!
Mitandao ya kijamii kama vile twitter na facebook
ni muhimu sana kwa watu wazima na vijana wanaoitumia, kwani ni fursa mpya za kuweza
kukutana na hatimaye, kujenga uhusiano mbali na mahusiano ya kimapokeo kama yanvyofahamika
kwa wengi. Vijana ni watumiaji wakubwa wa mitandao ya kijamii, wanaojenga urafiki
na mahusiano na watu wengi kwa wakati mmoja. Kanisa limetambua umuhimu na mchango
wa mitandao ya kijamii ndiyo maana linataka kuwekeza zaidi ili kusaidia mchakato wa
Uinjilishaji Mpya.
Hapa Kanisa linaangalia vyombo mbali mbali vya mawasiliano
ya kijamii vinavyoweza kutumiwa na Kanisa katika mchakato wa Uinjilishaji mpya. wajumbe
wa mkutano huu wa siku tatu wamepata pia nafasi ya kutembelea Kanisa kuu la Familia
takatifu, wakiongozwa na mhandisi Jordi Bonet aliyeonesha mwingiliano kati ya Liturujia
na na kazi za Uhandisi.