2013-11-09 14:34:53

Wagonjwa ni hazina ya maisha na utume wa Kanisa


Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 9 Novemba 2013 amewashukuru wanachama wa Umoja wa Kitaifa wa Wasafirishaji wa Wagonjwa Lourdes na kwenye madhabahu ya Kimataifa wakati huu, UNITALSI inapoadhimisha Miaka 110 tangu ilipoanzishwa, msaada mkubwa kwa ajili ya kuwasaidia wagonjwa kusoma na kumwilisha Injili ya Upendo na faraja!

Wanachama wa UNITALSI walioenea sehemu mbali mbali za Italia ni mfano wa upendo wa Kristo Msamaria mwema, unaowasukuma kuwaonjesha ndugu zao wagonjwa uso wa huruma na faraja! Baba Mtakatifu anawaalika kutokata tamaa wanapokabiliana na vizingiti vya maisha na uchovu, bali wapige moyo konde na kusonga mbele, wakijitolea muda wao, tabasamu na upendo kwa wagonjwa, kwani wao ni sura ya Yesu anayeteseka.

Maskini na hata maskini wa afya ni utajiri mkubwa kwa Mama Kanisa, changamoto kwa vyama vya kitume kupokea na kuurithisha utajiri huu kwa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Wagonjwa si mzigo kwa Jamii, kumbe UNITALSI inachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni alama ya kinabii kwa Jamii na Kanisa, ili kutoa utambulisho na nafasi ya wagonjwa ndani ya Kanisa. Wagonjwa washirikishwe katika maisha na utume wa Kanisa mahalia; kwani hawa ni mashahidi na vyombo vya Uinjilishaji.

Baba Mtakatifu anawataka wagonjwa kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa na kwamba, kila mgonjwa anao mchango wake maalum kwa Kanisa, katika ukimya na maisha ya sala, mwaliko wa kupokea kwa uvumilivu na furaha mateso na mahangaiko ya ugonjwa, kama hazina muhimu kwa maisha ya Kikristo.

Baba Mtakatifu anawashukuru wagonjwa kwa hija mbali mbali wanazofanya kwa heshima ya Bikira Maria mjini Lourdes na sehemu mbali mbali za dunia, mwaliko wa kujifunza tunza na umama wa Bikira Maria, daima wakiwa tayari kusikiliza na kutekeleza sauti ya Kristo kwa njia ya Bikira Maria, ambaye daima amekuwa mwangalifu katika kukidhi mahitaji msingi ya binadamu; daima yuko tayari kuwaombea watoto wake upendo na neema inayookoa. Anawaombea na kuwafariji katika shida na mahangaiko yao: kiroho na kimwili.







All the contents on this site are copyrighted ©.