2013-11-09 10:54:26

Uinjilishaji na tunu msingi za maisha ya kifamilia ni kati ya vipaumbele vya Maaskofu Katoliki Vietnam


Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam katika mkutano wake wa kawaida uliohitimishwa hivi karibuni, limewaandikia waamini na watu wote wenye mapenzi mema barua ya kichungaji inayokazia dhamana ya Kanisa katika Uinjilishaji na tunu msingi za maisha ya kifamilia nchini humo. RealAudioMP3

Maaskofu wanasema, Uinjilishaji Mpya unalichangamotisha Kanisa kutafuta mbinu na mikakati mipya ya shughuli za kichungaji ili kukabiliana kwa dhati na mmong’onyoko wa tunu msingi za maisha ya kiutu, kiroho na kijamii katika familia nyingini nchini Vietnam.

Mwaka 2014, Kanisa Katoliki nchini Vietnam litajikita zaidi katika Mikakati ya shughuli za Kichungaji kwa ajili ya Familia. Wazo hili linakwenda sambamba na nia ya Baba Mtakatifu Francisko ambaye ametangaza Maadhimisho ya Sinodi Maalum kuhusu Familia itakayofanyika mwezi Oktoba, 2014 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Changamoto za familia mintarafu Uinjilishaji”.

Maaskofu wanasema, Kanisa ni familia ya Mungu, Kanisa dogo la nyumbani na kwamba, wongofu wa kweli unapata chimbuko lake kutoka katika familia. Huu ni mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanajenga misingi itakayoiwezesha familia kuwa ni shule ya sala, umoja, upendo na mshikamano unaodhihirisha ushuhuda wa imani katika matendo kama sehemu ya mchakato wa Uinjilishaji wa Mpya.

Wazazi wanapaswa kutambua dhamana na wajibu wao katika malezi kwani wao ndio walimu wa kwanza wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Watambue kwamba, familia bora za Kikristo ni chemchemi ya miito mitakatifu ndani ya Kanisa. Familia goi goi, zinaweza kuzalisha wahudumu wa Injili waliokengeuka kwa kukosa dira na mwelekeo sahihi katika maisha kwani waswahili wanasema, samaki mkunje angali mbichi, akishakauka hakunjiki tena!

Baraza la Maaskofu Katoliki Vietnam katika barua yake ya kichungaji linaendelea kukazia umuhimu wa maandalizi ya kutosha kwa wanandoa watarajiwa, watakaoshiriki kwa ukamilifu maisha na utume wa Kanisa, wakitambua kwamba, wanawajibika katika mchakato wa ujenzi wa Fumbo la Kanisa, Jamii na Nchi yao katika ujumla wake. Kinzani na migogoro inayojitokeza katika maisha ya ndoa na familia, ni mwaliko kwa Kanisa Katoliki nchini humo kuendelea kufafanua maana ya ndoa kadiri ya Kanisa Katoliki, umuhimu na dhamana yake.

Jumuiya za waamini zitambue familia zinazokabiliwa na matatizo na changamoto za maisha, ili ziweze kuwasaidia kwa sala, mawazo na matendo, badala ya kuwalaani na kuwatenga kana kwamba, wao ni mzigo katika maisha na utume wa Kanisa. Familia zenye matatizo, migogoro na kinzani, zinapaswa kuonjeshwa upendo na moyo wa ukarimu.

Kutokana na mwelekeo kama huu, Maaskofu Katoliki wa Vietnam wanapenda kukazia majiundo ya awali na endelevu kwa Makleri, Watawa na Waamini walei wanaojihusisha kikamilifu katika kuwandaa wanandoa watarajiwa.

Maaskofu katika mikakati yao ya kichungaji kwa Mwaka 2014 hadi 2016 watajikita katika dhamana ya Uinjilishaji wa Parokia na Jamii. Maaskofu wanahitimisha barua yao ya kichungaji kwa kuwaomba Mashahidi wa Vietnam, ambao ni kielelezo makini cha Uinjilishaji wa kina, wawasaidie waamini kuishuhudia imani yao kwa Kristo kwa njia ya matendo.








All the contents on this site are copyrighted ©.