2013-11-09 09:57:06

Sera za utoaji mimba ni kutaka kupandikiza majanga kwa Jamii!


Baraza la Maaskofu Katoliki Angola, Sao Tome na Principe linasema, sera za utoaji mimba ni mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, ni kinyume cha Amri za Mungu; utamaduni na utambulisho wa wananchi wa Angola. Wananchi wanakumbushwa kwamba, maisha ya binadamu ni matakatifu tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Hakuna mtu mwenye mamlaka yanayomruhusu kuwapokonya wengine zawadi ya uhai kwa kisingizio chochote kile. Ni jukumu na dhamana ya wanafamilia, wahudumu wa sekta ya afya na wanasiasa kutoruhusu wala kushabikia sera za utoaji mimba na badale yake, wawe mstari wa mbele kulinda na kutetea zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Maaskofu wanasema kwamba, kadiri ya mila na tamaduni za wananchi wa Angola katika ujumla wao, vitendo vya utoaji mimba havikubaliki kamwe kwani ni kielelezo cha mkosi katika familia. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wenye mapenzi mema kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai, kwani sera dhidi ya Injili ya uhai ni kutaka kusababisha majanga katika Jamii.

Ni matumaini ya wananchi wa Angola kwamba, wabunge wao watasimama kidete kulinda na kutetea zawadi ya uhai na kamwe hawatakubali kushinikizwa ili kuunga mkono sera za utoaji na vizuia mimba.







All the contents on this site are copyrighted ©.