2013-11-09 09:12:15

Matukio ya uvunjifu wa haki, amani na utulivu yanazidi kushamiri nchini Kenya!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linaiomba Serikali ya Kenya kuhakikisha kwamba, ina imarisha ulinzi na usalama wa raia na mali zao hasa kufuatia wimbi kubwa la mauaji ya viongozi wa kidini pamoja na uchomaji wa Makanisa, mambo yanayoashiria kuanza kutoweka kwa misingi ya amani na utulivu miongoni mwa wananchi wa Kenya.

Ujumbe huu umetolewa na Askofu mkuu Zacchaeus Okoth, Mwenyekiti wa Tume ya haki na amani, Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, hivi karibuni kwa kuwahimiza wananchi wote wa Kenya kuwa macho dhidi ya watu wanaotaka kulitumbukiza taifa katika maafa na majanga. Maaskofu wanaipongeza Serikali kwa kuanzisha mchakato wa ulinzi shirikishi kutoka katika jamii.

Maaskofu wanasikitishwa sana na ongezeko la vitendo vya utekaji nyara wa watu na magari; vitendo vya kigaidi na mauaji ya kutisha. Maaskofu wanasema, amani na usalama viko mikononi mwao wenyewe, kumbe wanawajibika kulinda na kudumisha amani na usalama kwa ajili ya mafao ya wengi. Waamini wenye misimamo mikali ya imani wanapaswa kudhibitiwa ili wasiwe ni chanzo cha kuvunjika kwa haki msingi za binadamu na utawala bora. Serikali inawajibu na dhamana ya kulinda raia na mali zao.

Ni jukumu la waamini wa dini zote kutojihusisha na vitendo vya umwagaji damu kwa kisingizio cha masuala ya kidini. Mwelekeo wa namna hii ni kinyume kabisa cha mapenzi na utashi wa Mungu ambaye ndiye asili ya amani na utimilifu wa mema yote.

Maaskofu wanakemea kwa nguvu zote tabia ya rushwa na ufisadi; upendeleo na ukabila, inayoendelea kukua na kuimarika kwa kasi nchini Kenya. Wanasema, inasikitisha kuona kwamba, viongozi wa Serikali wanaendelea kujipatia mishahara na marupurupu makubwa wakati wananchi wengi wa Kenya wanatumbukia katika baa la ujinga, umaskini na magonjwa.

Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, linaitaka Serikali kuhakikisha kwamba, inajenga na kuimarisha umoja wa kitaifa, haki na amani; ustawi na maendeleo ya wengi. Rasilimali na utajiri wa Kenya uwe ni kwa ajili ya mafao ya wengi na wala si kwa ajili ya viongozi wachache!







All the contents on this site are copyrighted ©.