Zingatieni sura ya Mchungaji mwema, mnapotekeleza wajibu wa Kanisa kuinjilisha na
kutoa haki!
Mahakama kuu ya Vatican inao wajibu wa kusaidia shughuli za kitume zinazofanywa na
Makanisa mahalia katika mchakato wa kuhakikisha kwamba, haki ndani ya Kanisa inatendeka
kwa kutoa maamuzi sahihi. Ni mahakama inayopaswa kushirikiana bega kwa bega na Maaskofu
ili kuwawezesha kuwa kweli ni wahudumu wa amani.
Ubatilishaji wa ndoa za Kikristo
ni kati ya kazi nyeti inayotekelezwa na Mahakama kuu ya Vatican; utume ambao unawataka
wadau kutekeleza wajibu wao barabara, ili ukweli na haki viweze kutolewa kwa ajili
ya mafao ya shughuli za kichungaji kwa pande zote zinazohusika. Mahakama hii imekwisha
toa mchango mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, hasa zaidi katika maandalizi
ya Hati ya Kichungaji "Dignitas Connubii", "Heshima ya Wanandoa" inayotoa
sheria elekezi katika masuala ya ndoa.
Ni maneno ya Baba Mtakatifu Francisko
alipokutana na wajumbe wa Mahakama kuu ya Vatican wanaofanya mkutano wao wa Mwaka
kwa kuangalia kanuni na mikakati inayoweza kutumika kwa ajili ya kuimarisha mshikamano
wa ndoa katika mchakato wa sheria za Kanisa mintarafu ubatilishaji wa ndoa.
Baba
Mtakatifu anawataka wajumbe hawa kusimama kidete kulinda na kutetea mshikamano wa
wanandoa; kwa kuhakikisha kwamba, wanatafuta ushahidi ili kuhakiki madai yanayoletwa
mbele yao, kwa kuheshimu ukweli na mshikamano wa ndoa. Matatizo ya kiakili ni kati
ya mambo yanayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa, kumbe, wanapaswa kuwa makini katika
mambo haya; kwa kusoma na kupitia mwenendo mzima wa kesi husika bila kushinikizwa
na ukiritimba au masuala ya mpito! Wao wanapaswa kuwa ni wapatanishi kati ya Sheria
za Kanisa, hali ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.
Wao kama watetezi wa
sheria za Kanisa, wanayo dhamana ya kutoa maana ya kesi iliyoko mbele yao hata wakati
mwingine kwa kukata rufaa kwenye Mahakama kuu ya Rufaa ya Vatican, pale inapoonekana
kwamba, maamuzi yanakwenda kinyume cha ukweli dhidi ya mshikamano wa ndoa; mambo yanayohitaji
ushirikiano wa dhati katika maboresha ya shughuli hizi.
Baba Mtakatifu anasema,
Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, Kanisa ni kielelezo cha umoja,
kumbe hata mtetezi wa ndoa anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa kuzingatia mwelekeo
huu, kwa kuthamini, kuheshimu na kukuza majadiliano kati ya watu wanaohusika.
Baba
Mtakatifu Francisko anawaambia wafanyakazi wa Kanisa wanaoshughulikia utume wa haki
ya Kanisa, kutambua kwamba, wanafanya kazi hii kwa niaba ya Kanisa na kwamba, wao
pia ni sehemu ya Kanisa, kumbe, kuna haja ya kuweka uwiano makini kati ya Kanisa linaloinjilisha
na Kanisa linalotoa haki. Huduma ya kichungaji katika shughuli za haki ni dhamana
ya kitume inayopaswa kutekelezwa kwa kuzingatia ile sura ya Mchungaji mwema anayejitaabisha
kutafuta Kondoo aliyejeruhiwa na kupotea.
Mwishoni, Baba Mtakatifu anaendelea
kuwatia moyo katika utekelezaji wa utume wao kwa kuwa waangavu na wenye haki ndani
ya Kanisa, kama njia ya kupata majibu muafaka na shahuku ya waamini kwa viongozi wao
wa Kanisa, ili waweze kufafanuliwa hali yao ya maisha.