Tafakari ya Neno la Mungu, Jumapili ya 32 ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa
Mpendwa msikilizaji wa Neno la Mungu kipindi tafakari masomo Dominika, tayari tuko
katika Dominika ya 32 ya mwaka C wa Kanisa, ni Dominika ambayo kwayo tunafunga wiki
ambamo tuliwakumbuka na kuwaombea marehemu wetu.
Na kwa hakika
Neno la Mungu ambalo tunalitafakari Dominika hii lina jambo la pekee linalogusa marehemu
na nyakati za mwisho. Ujumbe wa Neno la Mungu kwa ufupi ni kwamba Mungu ni Mungu wa
wazima na si wa wafu.
Mpendwa msikilizaji, katika Injili tunayoitafakari tunakutana
na baadhi ya Masadukayo ambao kwa kawaida ni kikundi cha watu wanganganizi wa mila
zao, wasiosadiki katika ufufuko wa wafu, wenye kushika utawala wa pesa katika masinagogi
na mahekalu na kwa namna hiyo walikuwa wameshikamana na urka wa kikuhani. Watu hawa
mpendwa msikilizaji, wanaweka swali mbele ya Bwana, swali ambalo mantiki yake ni kutaka
kuangusha mafundisho ya Bwana juu ya UFUFUKO wa wafu!
Katika mantiki hiyo
Masadukayo wanakuja na hadithi amabayo hatuna uhakika kama ni ya kweli ama ni ya kutunga.
Hadithi yagusa mwanamke aliyeolewa na wanaume saba ndugu ambao walikuwa wakirithishana
kadiri ya sheria ya Musa na kadiri ya hadithi hiyo hakupata mtoto na wanaume hawa!
Kama kawaida naye mwisho alikufa. Sasa swali mtego kwa Bwana linakuja likisema huyu
mama katika ufufuo wa wafu atakuwa mke wa nani? Pamoja na hilo unaona jinsi ambavyo
Masadukayo ni wajanja, wanatumia Biblia kusimamia hoja yao!
Mpendwa mwana wa
Mungu, katika kujibu swali hilo, Bwana atahakikisha ukweli wa ufufuko na kisha atakemea
mtizamo wa Kisadukayo unaogusa ulimwengu wa vitu, badala ya ulimwengu wa ufufuko,
ulimwengu wa Kimungu. Bwana atasema mara moja kuwa katika ulimwengu ujao yaani ufufuko
kwa wale wateule wa Mungu, hakuna kuoa wala kuolewa, hakuna kifo tena bali wote watakuwa
kama malaika, na kwa vile ni wana wa ufufuko basi ni wana wa Mungu.
Katika
hili Bwana anaweka mbele yetu maisha mapya, maisha baada ya ufufuko uhakika wa imani
yetu. Ndiyo kusema maisha ya ufufuko si mwendelezo wa raha za kidunia, yaani kunywa
na kula bali ni maisha tofauti, yenye thamani tofauti. Ni kweli mwanadamu daima anasubiri
ukamilifu wa maisha yake lakini ni lazima atambue kuwa si mwendelezo wa mambo ya kidunia
bali ni zawadi ya kimungu, ni upendo upeo, mastahili ya msalaba wa Kristo.
Mpendwa
msikilizaji, jambo hili tulilosikia, laweza kupelekea kufikiri je kuna haja gani ya
kuwa na vifungo vya mapendo ya kindoa, kama haya mambo hayana nafasi katika ufufuko?
Kwa hakika haina maana kwamba kifungo cha mapendo kama hayo hakitakuwepo, bali kitakuwa
katika kipimo cha ukamilifu tofauti na kipimo cha leo! Katika barua ya Mtakatifu
Yohane twasoma “Wapenzi sasa tu wana wa Mungu, wala haijadhihirika bado tutakavyokuwa,
lakini twajua yakuwa atakapodhirishwa tutafanana naye, kwa maana tutamwona kama alivyo!
IYn 3:2.
Kumbe maisha ya mapendo tuyaishiyo hapa duniani yatakuwa katika ukamilifu
wake ambao hatuwezi kuutambua kwa macho bali kwa imani thabiti katika mausia ya Bwana.
Mpendwa
msikilizaji, Injili tunayoitafakari inagusa maisha ya mtu na hasa mashaka yake katika
maisha ya kila siku. Kwa hakika tangu karne za kwanza za Kanisa mpaka leo bado kuna
Masadukayo na bado kati yetu waamini na wasio waamini tunajiuliza hivi huyu ndugu
yangu aliyekufa ni kweli anawenda mbinguni? Je, ataendelea kunipenda kama ambavyo
ninafikiri mimi? Je mwili wake utaungana na roho, na ni kwa namna gani? Kwa uwepo
wa maswali haya kunafajionesha katika kulia na kuomboleza mmoja anapotoweka kwa njia
ya kifo, ndiyo kusema hatuzoei kifo!
Basi ndugu yangu mpendwa, katika sehemu
ya mwisho ya kifungu hicho cha Injili ya Luka, Bwana anajibu shida yetu sisi tulio
na imani akisema: lakini yakuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionesha katika sura
ya kijiti hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahim una Mungu wa Isaka na Mungu
wa Yakobo, naye si Mungu wa wafu bali wa walio hai! Mpendwa msikilizaji jambo
la ufufuko ni kiini na kilele cha imani yetu, imani ambayo ni mwanga. Ili kujenga
msimamo huo lazima mmoja ajenge uthabiti katika imani kama asemavyo Baba Mtakatifu
Francisko kuwa, Imani ni alama za maandalizi ya kuelekea katika mji wa ahadi unaoandaliwa
na Mungu kwa binadamu. Mji ambao ni wa wazima na si wa wafu. Na kwa kutambua hili,
tunaweza kuona kwamba, kwa kila binadamu imani humwangazia binadamu juu ya mahusiano
yake na Mungu na wanadamu wenzake. Kwa kusadiki namna hii kunatuondolea wasiwasi na
kutupa tumaini ya kwamba tutaurithi uzima wa milele. Tumsifu Yesu Kristo. Tafakari
hii imeletwa kwako na Padre Richard Tiganya, C.PP.S.