"Shuhudieni huruma ya Mungu na mjikite barabara katika majiundo ya majandokasisi"!
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe alioliandikia Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa
wakati huu wanapofanya mkutano wao wa Mwaka, mjini Lourdes, anawasihi kujitosa bila
ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa binadamu, lakini zaidi kwa maskini na wote wanaosukumizwa
pembezoni mwa Jamii.
Anawataka kujikita zaidi katika majiundo ya Majandokasisi
ili waweze kukita mizizi yao katika Kristo, tayari kujitoa bila ya kujibakiza kwa
ajili ya Mungu na jirani zao. Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika Maaskofu Katoliki
kuwa karibu zaidi na waamini waliokabidhiwa kwao na Kristo katika huduma za kichungaji.
Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Askofu mkuu George Pontier, Rais wa
Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa, anaishukuru Familia ya Mungu nchini humo kwa
kukuza na kuimarisha ari na moyo wa kimissionari, hali inayojionesha kwa namna ya
pekee katika Parokia za Kanisa Katoliki nchini Ufaransa. Waamini wanaalikwa kuendeleza
mchakato wa toba na wongofu wa ndani kama ushiriki wao makini katika Uinjilishaji
mpya unaodai ushuhuda wa imani tendaji.
Baba Mtakatifu anawashukuru pia Maaskofu
kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaofanya mikutano yao kama kielelezo cha mshikamano
wa Kiaskofu pamoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa ajili ya ustawi na maendeleo
ya Kanisa la Kristo.