2013-11-07 08:34:51

Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel kutangazwa kuwa Mwenyeheri, hapo tarehe 10 Novemba 2013


Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili ijayo tarehe 10 Novemba 2013, anatarajiwa kumtangaza Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel kuwa Mwenyeheri, katika Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa Jimboni Paderborn, Ujerumani.

Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel alizaliwa na kulelewa katika familia ya Kikristo. Wazazi wake walikuwa ni wachamungu na mfano bora wa kuigwa na jirani, kwani walijitahidi kujenga familia yao, ikawa ni Kanisa dogo la nyumbani, shule sala na utakatifu wa maisha.

Baada ya masomo yake ya msingi, "Aline" kama walivyozoea kumwita nyumbani kwao, alitamani sana moyoni mwake kuwa mtawa, lakini akakumbana na pingamizi kutoka kwa mama yake mzazi aliyekataa kuridhia ndoto yake na kwamba, dada yake alikuwa pia ni mgonjwa. Mahangaiko haya ya ndani yaliandamana naye katika safari ya maisha yake ya kiroho, hadi pale alipoaga dunia.

Mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel hakukata wala kukatishwa tamaa, aliendelea kubaki mwaminifu kwa ndoto yake ya kutaka kuwa mtawa kwa ajili ya Mungu na jirani zake. Kunako mwaka 1863 Askofu wa Jimbo la Paderborn, Ujerumani aliridhia wazo la Maria Teresa Bonzel na wenzake kuanzisha Shirika la Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko.

Shirika hili jipya likaitwa "Masista Fukara Wafranciskani Waabudu wa Daima". Sr. Bonzel alichaguliwa kuwa Mama mkuu wa Shirika hadi alipofariki dunia tarehe 6 Februari 1905. hadi kufariki kwake, Shirika lilikuwa na watawa 870 waliokuwa wanaishi katika nyumba 71 nchini Ujerumaini. Amerika, Shirika lilikuwa na watawa 700 waliokuwa wanaishi katika nyumba 42.

Maisha ya mtumishi wa Mungu Maria Teresa Bonzel yalisimikwa katika sala iliyomwilishwa kwenye matendo ya huruma anasema Kardinali Angnelo Amato. Ni mtawa aliyejiachilia mikononi mwa Mwenyezi Mungu wakati wa majanga ya maisha; wakati wa shida na karaha. Alikuwa na Ibada ya pekee kabisa kwa Yesu wa Ekaristi Takatifu, akaonesha upendo usiokuwa na mipaka kwa watoto waliokuwa wanaishi ndani na nje ya taasisi yake. Alihakikisha kwamba, watoto wengi zaidi wanapata hifadhi na usalama katika maisha yao kwa kuwakabidhi kwenye familia bora.

Mwenyeheri Maria Teresa Bonzel ni zawadi kubwa si tu kwa Shirika na Jimbo lake la Paderborn, bali hata kwa Kanisa zima, kwani ni kielelezo cha moyo uliokumbatia kwa dhati kabisa maneno ya Kristo, kiasi cha kuchanua na kutoa harufu safi ya ujasiri na utakatifu wa maisha unaojionesha katika imani tendaji. Lengo la kuwekwa kwake wakfu, lilikuwa ni kumsaidia katika mchakato wa kutafuta utakatifu wa maisha kwa kukumbatia Mashauri ya Kiinjili; muhtasari wa Mafundisho Makuu ya Yesu.

Ni mtawa anayeonesha jitihada za mwanadamu katika kumtafuta na hatimaye, kukutana na Mwenyezi Mungu, kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu na jirani zake wanaohitaji zaidi msaada wake. Na kwanjia hii akabahatika kufikia utimilifu wa maisha yake.

Hivi karibuni Baba Mtakatifu Francisko alisema kwamba, watakatifu kabla ya kuvishwa taji la utukufu na heshima, walikuwa ni watu wa kawaida, waliokumbuna na majanga, furaha na matumaini katika maisha yao ya kila siku. Ni watu walioonja upendo wa Mungu uliowawezesha kuleta mageuzi katika maisha yao, wakaamua kujitosa kimasomaso kwa ajili ya Mungu na jirani; wakasambaza harufu nzuri ya matendo ya huruma, furaha na amani.

Waamini wanakumbushwa kwamba utakatifu wa maisha si upendeleo kwa ajili ya watu wachache, bali ni wito na mwaiko kwa wote. Sakramenti ya Ubatizo inamkirimia mwamini neema katika imani, matumaini na mapendo; ili kukua na kukomaa katika utimilifu wa maisha ya Kikristo, kwa kupokea na kutekeleza mapenzi ya Mungu katika hija ya maisha yake ya kila siku! Hii ndiyo changamoto iliyoko mbele ya kila mwamini anasema Kardinali Angelo Amato.









All the contents on this site are copyrighted ©.