Komesheni kinzani, migogoro na vita ili watu wajikite katika mchakato wa maendeleo
endelevu!
Viongozi Barani Afrika hawana budi kusimama kidete kulinda na kutetea haki msingi
za binadamu, amani na utulivu sanjari na kuponya makovu ya chokochoko na kinzani za
kidini, kisiasa na kijamii, ili kuzuia majanga yanayoendelea kujitokeza kwa wakimbizi
na wahamiaji kutoka Barani Afrika kujikuta wanakufa maji, katika harakati za kutafuta
usalama na ubora wa maisha ughaibuni!
Utawala bora, mikakati makini ya maboresho
ya uchumi na maisha ya kijamii ni mambo msingi ambayo yanaweza kulisaidia Bara la
Afrika kujinasua kutoka katika lindi la umaskini, magonjwa, njaa na vita. Huu ni mchango
uliotolewa na wajumbe wa tume ya haki na amani kutoka Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu
katoliki Afrika na Madagascar, SECAM katika mkutano wake wa Mwaka uliohitimishwa hivi
karibuni mjini Bujumbura, Burundi.
Wajumbe hawa wanasema, kuna ongezeko kubwa
la biashara haramu ya binadamu na viungo vyake kutoka Barani Afrika. Baadhi ya nchi
bado zinaendelea kukabiliana na kinzani, migogoro na vita inayojikita katika masuala
ya: ukabila, udini, uchu na uroho wa madaraka. Baadhi ya viongozi Barani Afrika wameendelea
kufumbia macho chokochoko za kidini kwa baadhi ya waamini wenye misimamo mikali ya
kidini kufanya mashambulizi dhidi ya raia wengine, bila ya kufikishwa kwenye mkondo
wa sheria. Haya ndiyo yanayojitokeza nchini Nigeria, Mali, Misri, Somalia, Kenya na
Tanzania.
Kuna baadhi ya viongozi wa Serikali wanashirikiana na makampuni makubwa
kutoka ndani na nje ya Bara la Afrika kwa ajili ya kunyonya utajiri na rasilimali
ya Afrika kwa ajili ya mafao ya watu wachache, wakati kundi kubwa la raia wakiendelea
kuogelea katika dimbwi la ujinga, umaskini na maradhi. Wajumbe hao wanaitaka Mamlaka
ya Bonde la Mto Nile, kutambua kwamba, kuna mamillioni ya watu yanategemea ustawi,
maisha na maendeleo yao kutokana na maji ya Mto Nile, kumbe maamuzi yoyote yanapaswa
kuzingatia kwanza mafao ya wengi kwa njia ya majadiliano ya kina!