Jitoeni kimasomaso kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na utulivu!
Wajumbe wa mkutano mkuu wa kumi wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni wameendelea kujadili
pamoja na mambo mengine, kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea na kudumisha
misingi ya haki na amani duniani. Itakumbukwa kwamba, mkutano huu unaongozwa na kauli
mbiu "Mungu wa uhai, tuongoze katika misingi ya haki na amani.
Haki inayotafutwa
inapaswa kujidhihirisha katika medani mbali mbali za maisha ya mwanadamu: kwa mfano
katika sekta ya uchumi, fedha na biashara kwa kuhakikisha kwamba, wadau wanawajibika
kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima na maisha ya mwanadamu. Makanisa hayana
budi kuwezeshwa kikamilifu ili kupambana na majanga katika maisha ya mwanadamu pamoja
na kutunza mazingira.
Maadili ya kazi na utume wema ni kati ya vipaumbele
vinavyokaziwa na wajumbe wa mkutano mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni huko Busan,
Korea ya Kusini. Kufilisika kwa Mabenki na Makampuni makubwa kutoka Ulaya na Amerika
ni chanzo kikubwa cha athari za myumbo wa uchumi kimataifa unaoendelea kusababisha
majanga kwa mamillioni ya familia duniani, kiasi kwamba, hata wale wanaoishi katika
nchi zinazoendelea sasa wanaanza kuonja makali ya athari za myumbo wa uchumi kimataifa.
Jamii
inapaswa kuwaangalia wanyonge na watu wenye ulemavu, kama sehemu ya mchakato wa kulinda
na kutetea zawadi ya uhai kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, vijana wapewe fursa
za ajira ili waweze kukabiliana na maisha kikamilifu. Makanaisa yaendelee kuwa mstari
wa mbele katika mapambano dhidi ya uvunjifu wa haki msingi za binadamu, dhuluma, nyanyaso
na ubaguzi wa rangi. Makampuni makubwa yanayowekeza vitega uchumi vyake katika nchi
changa zaidi duniani yasaidia kuchangia mchakato wa maendeleo endelevu na maboresho
ya maisha ya watu katika elimu na afya.
Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutambua
kwamba, upendo ni chemchemi ya haki, amani, utulivu na maendeleo. Watu wanapaswa kujenga
na kuimarisha mapendo kati yao na mazingira, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri
zaidi pa kuishi. Huduma bora za afya ni sehemu ya haki, Serikali na wadau mbali mbali
wahakikishe kwamba, haki hii inawafikia watu wengi zaidi badala ya kujikita kutafuta
faida kubwa kwa gharama ya maisha ya watu wanyonge!
Wajumbe wa Baraza la Makanisa
Ulimwenguni wanatambua na kuheshimu mchango wa wanawake Wakristo katika ustawi na
maendeleo ya Makanisa ulimwenguni. Wanataka wanawake hawa wawezeshwe kwa hali na mali
ili waendelee kuchangia zaidi katika maendeleo ya Makanisa mahalia. Kuna haja ya kuendelea
kuhimiza mikakati ya kilimo cha kisasa na utunzaji bora wa mazingira, ili kupambana
na athari za mabadiliko ya tabianchi.