Bagamoyo ni ishara ya moyo uliopondeka na kuvunjika; kielelezo cha mwanga na matumaini
mapya katika Kristo!
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linapojiandaa kwa ajili ya Maadhimisho ya Kufunga
Mwaka wa Imani, hapo tarehe 10 Novemba 2013 mjini Bagamoyo, Askofu mkuu Josephat Lebulu
wa Jimbo kuu la Arusha katika mahojiano na Radio Vatican anasema kwamba, mji wa Bagamoyo
ni kielelezo cha moyo uliopondeka na kuvunjika kutokana na dhuluma, nyanyaso na madhara
makubwa ya biashara ya utumwa duniani.
Bagamoyo ni
Mlango wa Imani kwa Kanisa la Afrika Mashariki, kwani Wamissionari wa kwanza kujitosa
kimasomaso kutangaza Habari Njema ya Wokovu walitua nanga ya matumaini ya watu mjini
Bagamoyo. Hapa mwanadamu akapata matumaini na mwanga mpya wa maisha, kiasi cha kuanza
kutembea katika uhuru na mwanga wa Kristo Mfufuka. Bagamoyo ukageuzwa na kuwa ni kielelezo
cha maisha mapya katika Kristo na kinzani katika hija ya imani.
Askofu mkuu
Lebulu anasema kwamba, Bagamoyo imekuwa ni ishara ya upinzani na tumaini jipya; mwanga
mpya wa maisha badala ya kukata tamaa. Licha ya Bagamoyo kuwa ni Mlango wa Imani ya
Kikristo, lakini bado mji huu umebaki nyuma katika maisha ya Kikristo, lakini watu
wameufahamu mpango wa Mungu unaopania kuwakomboa wote! Kumbe, Bagamoyo unabaki kuwa
ni Mlango wa Imani na Mwanga wa matumaini mapya.