2013-11-06 09:02:49

Mchakato wa Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia, 5-19 Oktoba 2014


Maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi Maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia itakayofanyika kuanzia tarehe 5 hadi tarehe 19 Oktoba 2014 kwa kuongozwa na kauli mbiu "changamoto za kichungaji ndani ya familia mintarafu mchakato wa Uinjilishaji", yameanza na tayari hati ya maandalizi ya Sinodi hii imewasilishwa kwa wadau mbali mbali ili waanze kuifanyia kazi na kutuma mchango wao kwenye Sekretarieti ya Sinodi mwishoni mwa Mwezi Januari, 2014.

Hayo yamebainishwa na viongozi wakuu wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia wakati walipokuwa wanazindua rasmi hati ya kufanyia kazi. Askofu mkuu Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia anasema kwamba, Sinodi hii inapenda kutafsiri kwa namna ya pekee, mawazo na nia za Baba Mtakatifu Francisko kama sehemu ya mchakato wa kukabiliana na changamoto za kichungaji mintarafu maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla.

Maadhimisho ya Sinodi hii yatafanyika katika awamu kuu mbili: Awamu ya Kwanza ni kwa ajili ya kusikiliza shuhuda kutoka kwa Maaskofu katika mchakato wa kutangaza na kuishi kwa uaminifu Injili ya Familia. Awamu ya Pili ya Maadhimisho ya Sinodi hii yatafanyika mwaka 2015 kwa kutoa fursa kwa Mababa wa Sinodi kuibua mbinu mkakati wa kichungaji kuhusu binadamu na familia. Wadau na wahusika wakuu katika Maadhimisho ya Sinodi hii wamekwishapelekewa Hati ya Maandalizi ya Sinodi.

Lengo la Baba Mtakatifu Francisko ni kuhakikisha kwamba, Maaskofu wanajenga na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao katika kukabiliana na changamoto za kichungaji, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, mawazo ambayo kwa sasa yanapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Pili, Baba Mtakatifu anapenda kuimarisha dhamana na kazi ya Sekretarieti ya Sinodi ya Maaskofu inayofanya kazi bega kwa bega na Khalifa wa Mtakatifu Petro katika utekelezaji wa majukumu yake. Haya ni kati ya mabadiliko makubwa anayopania Baba Mtakatifu kwa sasa kwa ajili ya mafao na maendeleo ya Kanisa la Kiulimwengu.

Askofu mkuu Baldisseri anasema, mmong'onyoko wa tunu msingi za maadili, maisha ya kiroho na utu wema katika ulimwengu mamboleo ni mambo yanayohitaji mikakati makini ya shughuli za kichungaji. Sinodi hii itawahusisha viongozi mbali mbali wa Kanisa. Hati ya Maandalizi ya Sinodi ina utangulizi wa jumla, Mafundisho ya Biblia kuhusu Familia, Mafundisho ya Viongozi wa Kanisa pamoja na maswali dodoso yanayopaswa kuangaliwa na kujibiwa kwa ukamilifu na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia.

Majibu ya Maaskofu yatatumwa kwa Sekretarieti ya Sinodi mwishoni mwa Mwezi Januari, 2014 na kufanyiwa kazi na Sekretarieti ya Sinodi mwezi Februari, ili kutengeneza "Hati ya Kutendea Kazi" Yaani, Instrumentum Laboris kwa ajili ya Mababa wa Sinodi.

Kardinali Peter Erdo, Mwezeshaji mkuu wa Maadhimisho ya Sinodi ya tatu ya Maaskofu kwa ajili ya Familia amegusia kwa muhtasari yale yaliyojiri kwenye Hati ya ya Maandalizi kwa ajili ya Maadhimisho ya Sinodi na kwamba, inajikita zaidi katika mambo msingi ya Sheria za Kanisa na mwelekeo wa shughuli za kichungaji mintarafu maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Sehemu ya pili ya hati hii inazungumzia Kanisa na Injili ya Familia kwa kujikita zaidi na zaidi kwenye Maandiko Matakatifu, taalimungu, maisha ya kijamii na kisheria. Sehemu ya tatu ni maswali dodoso yanayogusa maswala nyeti na tata katika maisha na utume wa Familia nyakati hizi.

Mama Kanisa anapenda kuipembua dhana ya Familia mintarafu maisha ya ndoa, kwa kutambua kwamba, Familia ipo kwa sababu imenuiwa na Mwenyezi Mungu mintarafu sheria maumbile, uhuru wa mtu unaoongozwa na dhamiri nyofu ambayo kimsingi ni sheria ya Mungu katika undani wa mwanadamu. Kumbe, Ndoa na Familia ni sawa na chanda na pete anasema Kardinali Erdo. Hii inatokana na ukweli kwamba, mwanaume na mwanamke wanakamilishana katika mapendo kamili, wakiwa tayari kupokea zawadi ya watoto kutoka kwa Mungu. Ndiyo maana Maaskofu wanaulizwa kuhusu sheria za nchi zao kuhusiana na masuala ya ndoa.

Maswali dodoso yanawachangamotisha waamini kutoa maoni yao kuhusu sheria maumbile ya uhusiano kati ya bwana na bibi, ili kuweza kupata majibu muafaka kuhusu ndoa zinazofungwa Kiserikali kwa kutambua umuhimu wa familia katika maisha na utume wa Kanisa na Jamii kwa ujumla kama walivyofafanua Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Kanisa linapenda kuangalia pia changamoto zinazoendelea kujitokeza katika familia hasa kutokana na ubinafsi na uhuru usiokuwa na mipaka, kiasi hata cha kwenda kinyume na maumbile pamoja na mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Wanandoa wanapaswa kuwa waaminifu kwa mpango wa Mungu katika maisha ya ndoa na familia, kwa kujitahidi kufahamu Mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia, kama yalivyofafanuliwa na Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki na Sheria za Kanisa na Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican. Wanandoa watambue umuhimu wa Sakramenti ya Ndoa na masharti yake, kwa kuonesha dhamiri nyofu.

Ndoa miongoni mwa wabatizwa ni Sakramenti ya umoja na mapendo yasiyogawanyika. Ndiyo maana kwenye maswali dodoso, Maaskofu wanaulizwa kuhusu maandalizi ya wanandoa watarajiwa katika Majimbo na Parokia zao na jinsi ambavyo wanandoa wanaweza kusaidiwa na Parokia pamoja na vyama vyao vya kitume! Ndoa za watu wa jinsia moja zinazungumziwa pia katika maswali dodoso, kwani hili ni kati ya maswali na hali tete inayozikabilia familia nyingi katika nchi zinazoendelea. Hali hii inahitaji kufanyiwa tafakari ya kina ili kuibua majibu muafaka katika maisha na utume wa Ndoa na Familia.

Wanandoa walioachika na kuamua kuoa au kuolewa tena ni kati ya changamoto za shughuli za kichungaji kwa wakristo wengi, kwani kati yao kuna wale wanaodhani kwamba, wanatengwa na Kanisa kutokana na kutoshirikishwa maisha ya Kisakramenti hasa Sakramenti ya Upatanisho na Ekaristi Takatifu, kiini cha maisha ya ndoa katika mchakato unaopania utakatifu wa maisha! Maswali dodoso yanaangalia pia jinsi ambavyo mchakato wa kubatilisha ndoa unavyoweza kuharakishwa; elimu na malezi ya watoto ndani ya familia na umuhimu wa Mapadre kuwa waaminifu kwa masharti ya maungano kadiri ya sheria na kanuni za Kanisa.

Kardinali Peter Erdo anasema kwamba, Jamii inapaswa kutambua kwamba, Familia ni zawadi ya pekee kabisa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa, ili iweze kutekeleza wajibu na dhamana yake ndani ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake.

Askofu mkuu Bruno Forte, Katibu mkuu maalum wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia anasema, Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kukazia kwa namna ya pekee, umoja na mshikamano miongoni mwa Maaskofu Katoliki kutoka sehemu mbali mbali za dunia katika maisha na utume wa Kanisa mintarafu Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Anataka kujenga na kuimarisha utamaduni wa Mama Kanisa kusikiliza kwa makini kilio cha watoto wake ili kukabiliana kwa ujasiri mkubwa na changamoto zinazojitokeza katika maisha na utume wa Familia ndani ya Kanisa na Jamii kwa ujumla, daima kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa mafao, ustawi, maendeleo ya familia, utu na heshima ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kufanya hija na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika maisha na utume wa Kanisa.

Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia inatoa kipaumbele cha kwanza katika mchakato wa Uinjilishaji kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya Wokovu inayotumwa kutangaza Injili ya Kristo kwa watu wote. Baba Mtakatifu anawaalika Maaskofu kuangalia umuhimu wa familia na changamoto zake katika ulimwengu wa utandawazi, ili kuokoa roho za watu na kulijenga Kanisa; kwa kutangaza kwa ari na mwamko mpya Injili ya Familia. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kukabiliana na changamoto za mmong'onyoko wa tunu msingi za maisha adili na utu wema.

Mama Kanisa anapaswa kusikiliza kwa makini matatizo na matumaini ya familia kutoka sehemu mbali mbali za dunia; ili familia iweze kupendwa na kuthaminiwa tena; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa zawadi ya maisha, utu na heshima ya binadamu. Familia ni shule ya ubinadamu uliotajirishwa, mwaliko kwa waamini kujitaabisha kuyafahamu Mafundisho ya Kanisa kuhusu ndoa na familia ili kugundua utashi wa Mungu uliofunuliwa kwa njia ya Yesu Kristo.

Ukarimu na huruma ni mambo ambayo Baba Mtakatifu Francisko anayapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni tunu wanazopaswa kumegewa wale ambao wana madonda ya maisha ya ndoa na familia. Injili ya Familia inapaswa kuhubiriwa kwa wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii, ili waonje huruma na upendo wa Mungu unaokoa na kuponya!

Askofu mkuu Bruno Forte anakiri kwamba, changamoto za maisha na utume wa familia katika ulimwengu mamboleo ni nyingi na ni tete kabisa! Ndoa za watu wa jinsia moja; haki ya malezi kwa watoto; maana ya familia na ndoa yenyewe! Udumifu na uaminifu wa wanandoa; Myumbo wa maisha ya kiimani kwa wanandoa walioachana na kuamua kuoa au kuolewa tena.

Zote hizi ni changamoto za kichungaji kwa sasa. Mama Kanisa anawaalika watoto wake wote kwa unyenyekevu na moyo mkuu kusindikiza mchakato wa maandalizi ya Maadhimisho ya Sinodi maalum ya Maaskofu kwa ajili ya Familia kwa njia ya Sala na Sadaka yao, ili Roho Mtakatifu aweze kuwaangazia waamini yale yanayofaa kwa ajili ya kutoa ushauri kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hati hii ya Maandalizi ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Familia imehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa. C.PP.S.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.







All the contents on this site are copyrighted ©.