Biashara haramu ya binadamu inaongezeka kwa kasi nchini Uingereza!
Wadau wanaopambana dhidi ya biashara haramu ya binadamu kutoka Uingereza wanasema
kwamba, biashara hii pamoja na biashara haramu ya viungo vya binadamu inaendelea kushamiri
katika nchi zinazoendelea duniani kutokana na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka.
Kuna baadhi ya watu ndani ya Jamii wanatumia umaskini wa wananchi kwa ajili
ya kuwarubuni na hatimaye, kuwatumbukiza katika biashara haramu ya binadamu. Vyombo
vya ulinzi na usalama nchini Uingereza vinaendelea kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana
na kundi la watu linalojihusisha na biashara haramu ya binadamu. Inasemekana hivi
karibuni, mtoto aliyetekwa nyara kutoka Somalia, alikamatwa nchini Uingereza, akiwa
kwenye mchakato wa kunyofolewa viungo vyake ili viweze kuuzwa kwenye soko la magendo!
Mashirika
yasiyo ya kiserikali yanayoongoza mapambano dhidi ya biashara haramu ya watoto, picha
za ngono na utalii wa ngono wanasema, mambo haya yananyanyasa na kudhalilisha utu
na heshima ya watoto hawa na kwamba, vitendo hivi vinaendelea kuongezeka kwa kasi
kubwa nchini Uingereza. Takwimu zinaonesha kwamba, ongezeko hili limefikia asilimia
50% tangu mwaka jana. Jeshi la Polisi Uingereza linasema kwamba, watoto 371 wametumbukizwa
katika utalii wa ngono. Wengi ya watoto hawa ni wale wanaotoka Vietnam, Nigeria, China,
Romania na Bangaladesh. Idadi hii inachafuliwa pia na uwepo wa watoto 20 kutoka Uingereza.