Wanafunzi wanaotumwa na Maaskofu, Wakuu wa Mashirika na Vyama vya Kitume kuja Roma
ili kujinoa wanapaswa kutambua kwamba, wao ni wawakilishi wa Kanisa la Afrika, wametumwa
ili kunoa akili zao, tayari kulitumikia Kanisa la Afrika kadiri ya mpango wa Mungu
katika maisha yao na wala si vinginevyo.
Wosia huu
umetolewa na Mheshimiwa Padre Alcuini Nyirenda, OSB wakati wa hafla ya kuwakaribisha
Wanafunzi Wakatoliki kutoka Tanzania waliofika hivi karibuni tayari kuanza safari
ya maisha ya ughaibuni, hapo tarehe 3 Novemba 2013, kwa ajili ya kujipatia ujuzi,
maarifa na stadi za maisha. Wanafunzi wamekumbushwa kutambua kwamba, wao ni tegemeo
la Kanisa Barani Afrika kwa sasa na kwa siku za usoni.
Muda wa masomo, kiwe
ni kipindi cha kujifunza kwa bidii, juhudi na maarifa, lakini wasiwe na matumaini
makubwa katika maisha kwa kudhani kwamba, baada ya masomo yao, basi watakuwa "watu
fulani katika Kanisa na Jamii katika ujumla wake". Mawazo kama haya yatawafanya waendelee
kuwa wafupi wa kimo kama ilivyokuwa kwa Zakayo mtoza ushuru anayesimuliwa katika Injili
ya Jumapili iliyopita.
Padre Nyirenda amewakumbusha wanafunzi hawa kwamba,
wanapohitimu masomo yao na kurudi nyumbani, watambue kwamba, Kanisa lina malengo na
mikakati yake ya shughuli za Uinjilishaji, kumbe malengo binafsi yasiwe ni kikwazo
kwa lengo kuu ambalo linapata chimbuko lake kutoka kwa Mungu mwenyewe. Jambo la msingi
kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajitosheleza wenyewe katika ukweli na utumilifu
wa maisha yao kama binadamu. Kila mtu ajitambue na kujitahidi kuwa mwenyewe! Ni mwaliko
wa kuonesha ukomavu katika maisha, Mwenyezi Mungu akipewa kipaumbele cha kwanza.
Wasomi
wanatakiwa kushirikiana na Mwenyezi Mungu katika mchakato wa kumletea mwanadamu ukombozi
wa kweli na maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.
Daima katika maisha yao wajitahidi kumwilisha, upendo kwa Mungu na jirani, hii ndiyo
kanuni msingi kwa ajili ya mafanikio katika maisha ya kila mwamini.