2013-11-05 09:56:31

Upendo kwa Mungu na jirani ndiyo lugha inayokoleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya!


Askofu mkuu Antonio Ariotti, Balozi wa Vatican nchini Paraguay katika hotuba yake kwenye mkutano wa 198 wa Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay, amelishukuru Kanisa Katoliki Amerika ya Kusini, kwa kulizawadia Kanisa la kiulimwengu Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa, anajitahidi kuendeleza mchakato wa Uinjilishaji mpya kwa njia ya maisha, maneno na matendo yake yanayogusa sakafu ya mioyo ya watu wengi duniani.

Mama Kanisa bado anaendelea kuchangamotishwa na Kristo kuubeba Msalaba kama kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake katika hija ya kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu sanjari na kuwaimarisha waamini katika imani yao kwa Kristo na Kanisa lake. Huu ni mwendelezo wa Maadhimisho ya Mwaka wa Imani, uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto wa kumi na sita, ukaendelezwa na Papa Francisko kwa ari na moyo mkuu!

Mwaka wa Imani, kimekuwa ni kipindi cha kugundua tena na tena zawadi ya imani kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili iweze kuwa ni taa na dira inayomwangazia mwanadamu katika maisha na vipaumbele vyake kwa njia ya maneno, lakini kwa kujikita zaidi katika matendo ya huruma, kielelezo makini cha imani tendaji kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Upendo kwa Mungu na jirani ndiyo lugha inayokoleza mchakato wa Uinjilishaji Mpya.

Askofu mkuu Antonio Ariotti amelipongeza Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay kwa kujiwekea mikakati ya maisha na utume wa Kanisa katika kukuza na kudumisha misingi bora ya maisha ya ndoa na familia, mwelekeo unaokwenda sanjari na nia ya Baba Mtakatifu Francisko katika kuitisha Sinodi Maalum ya Maaskofu itakayojadili changamoto za kichungaji katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya, Sinodi ambayo itaadhimishwa Mwezi Oktoba 2014.

Anasema, Paraguay inapaswa kujiwekea mikakati na mbinu makini zitakazowasaidia wananchi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho katika sekta ya elimu, afya, maendeleo endelevu, amani na utulivu. Ni dhamana ya Maaskofu kuwajengea waamini na wananchi uwezo wa kufanya majadiliano ya kina kwa ajili ya mafao ya wengi; lakini zaidi katika mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi; wananchi hawana budi kusimama kidete kupinga kwa nguvu zao zote mambo yanayopelekea ukosefu wa amani, utulivu na usalama kwa kuzingatia utawala wa sheria.

Wananchi wanapaswa kupambana kufa na kupona dhidi ya mambo yote yanayopelekea ukosefu wa haki msingi za kijamii; rushwa na ufisadi; ubaguzi na ukosefu wa fursa za ajira miongoni mwa vijana. Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay linaendelea kuufanyia kazi ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko aliowapatia Maaskofu wa Amerika ya Kusini kuhusu mwelekeo wa Kanisa kwa siku za usoni. Wanajadili pia mambo msingi katika maisha na utume wa Kanisa nchini humo.







All the contents on this site are copyrighted ©.