2013-11-05 09:22:57

MWUCE inavyokabiliana na changamoto za maboresho ya elimu nchini Tanzania


Hotuba ya Principal kwenye mahafali ya sita ya Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Cha Chuo Kikuu cha Mt. Augustino cha Tanzania) Mwenge- 02-11-2013
1 Utangulizi
Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Chuo, sisi wana Mwenge tunaona fahari sana kuwa nawe siku hii ya leo katika kuadhimisha Mahafali ya Sita ya Chuo chako hiki. Karibu sana Baba Askofu. Aidha naomba kuchukua fursa hii kukupongeza Baba Askofu kwa kuteuliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na hivyo pia kuwa Mkuu wa Chuo cha Mtakatifu Tanzania. Pongezi sana Baba Askofu. Huo ni wajibu mkubwa unaodai muda na majitoleo mengi licha ya kuwa na jimbo lako mwenyewe. Tunakuhakikishia sala zetu sisi wana Mwenge ili ujaliwe afya na nguvu ya kuendeleza wajibu hizo nyingi.

Mhashamu Baba Askofu Mkuu wa Chuo, Chuo cha Mwenge kimesimikwa katika mtazamo kwamba elimu ni taa ya kuangaza ili watu waweze kuona na kwa kuona waweze kupiga hatua na kusonga mbele. Mwasisi wa chuo hiki kwa kutambua kwamba elimu ni mwanga alichagua KAULI MBIU yake kuwa ni LUX MUNDI kwa Kiswahili MWANGA WA DUNIA ili iwe changamoto katika jitihada ya shughuli za chuo za kila siku kumwangazia mwanadamu aweze kupiga hatua ambazo zitamletea ufanisi katika maisha yake na yale ya jamii anayotazamia kuihudumia.

Mheshimiwa Mgeni Rasmi Chuo kimeendelea kusimamia azma hiyo ya kumtayarisha Mtanzania mtaalamu ambaye yuko tayari kuhudumia Watanzania wenzake kwa kutumia maarifa aliyopata kwa weledi na kwa uadilifu.

Chuo kilianza kama chuo cha ualimu yakiwa ni matayarisho ya kuwa chuo kikuu. Julai 2005 chuo kilipata usajili kuwa Chuo Kishiriki cha Mt. Augustino Tanzania. Chuo kinaendelea kukua kwani programu zinazofundishwa chuoni hapa zimeendelea kuongeza mwaka hadi mwaka. Kutoka Programu ya Ualimu wa masomo ya Sayansi iliongezwa programu ya Ualimu wa masomo ya Sanaa kwa sasa tunazo programu 24......zinazojumlisha programu za astashahada na shahada za uyamili. Programu hizo zimelenga katika kutoa elimu kwa maeneo maalumu ambayo jamii ya Kitanzania yanahitaji kwa sasa. Programu hizo zinajumlisha uhasibu, sheria, computa science, Geografina na mazingira, Sociology and social work, Mathematics and Statiscs na Ualimu kwa ngazi za shahada ya kwanza na shahada ya Uzamili.
2 Mahafali
Mhashamu Baba Askofu, Chuo cha Mwenge leo kinaadhimisha Mahafali ya Sita kama Chuo Kikuu Kishiriki cha Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Tanzania. Ni adhimisho la pekee kwa sababu kwa mara ya kwanza Chuo kinahitimsha wanachuo waliosomea Ualimu katika ngazi ya shahada ya Uzamili...ambao idadi yao ni kumi na moja. Jumla ya wahitimu wote ni 465....................

Hakuna shaka kwamba siku hii ni ya pekee sana kwa wahitimu wetu. Tunawapongeza kwa juhudi waliyoiweka hadi kufikia siku hii. Tunaposherehekea nao watambue kwamba tunamatazamio makubwa kwao kwamba wataenda kuishi kile ambacho wamejifunza hapa Chuoni. Uhakika wana jumuiya wa MWUCE waiona nao ni kwamba wahitimu waliotangulia wamekuwa wanafanya vema kazini kwa kuwa wengi wao wameonesha kuzingatia mafunzo waliopata. Nanyi tunawaasa mwende mkahudumie jamii ya Watanzania kwa kuwajali na kuweka mbele maslahi yao.

Aidha muwapo kazini kumbekeni kwamba utaalamu daima unadai kuendelea kusoma ili kujiimarisha katika fani na kupata maarifa mapya. Tafadhali dhana ya kwenda kwenye warsha au semina ili kupata malipo tuachane nayo...tutazame mbele na kuona umuhimu wa kuongezea maarifa ili uweze kufanya kazi yako vizuri zaidi. Kwa masikitiko makubwa utamaduni wa kutafuta semina au warsha kwa ajili ya malipo umejikita sana katika jamii – kuendeleza huo ni kuua taaluma na hata utendaji unakuwa hafifu kwani kunakuwa hakuna kujishughulisha katika kutafuta elimu zaidi itakayoinua viwango na kuimarisha utendaji.

Muwe mfano wa kuigwa katika kufanya kazi kwa juhudi na uelewa. Ijue fani yako na uiimarishe.
4 Mtaalamu wa Kitanzania
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, wajibu wa shule na vyuo ni kufundisha wanafunzi ili wakue katika maarifa na ujuzi. Chuo cha Mwenge kinatambua wajibu wake wa kukuza vipaji kwa kuwatayarisha wanachuo kuwa wataalamu mahiri katika maeneo ya ujuzi waliyoyachagua. Utaalamu unadai uwepo wa nia thabiti ya kulijua somo kwa kulisoma kwa bidii na kulenga kujiimarisha katika taaluma yenyewe. Wanachuo wanakumbana na changamoto nyingi zikiwemo za kukosa uwezo wa kiuchumi na hivyo kusoma kwa shida hasa kwa wale wasiokuwa na mikopo ya serikali, wengine wanakuwa na majukumu ya kusomesha wadogo zao au ndugu zao wakati wenyewe wanasoma na hata wengine wanakuwa hawajatulia na kuamua kwamba wanataka kujikita katika kusoma badala ya kuhangaika na maisha ya mitaani na kusoma.

Chuo kinafanya jitihada kuona kwamba wanachuo wanaojidahili kwenye Chuo cha Mwenge wanazingatia masomo na kufuata maelekezo na taratibu za Chuo kama zilivyopangwa na uongozi wa chuo. Miongozo hiyo imewekwa ili kuhakikisha kwamba mwanachuo anaongozwa kwa utaratibu utakaomwezesha kukabiliana na mazingira anayoenda kufanyia kazi na pia kuwa tayari kuingia kwenye mashindano ya soko la ajira nchini na hata nje ya nchi. Inabidi tukiri kwamba sehemu Fulani ya maandalizi ya wataalamu wetu inakumbwa na kigugumizi – kwa mfano: Kwa sehemu kubwa mazingira ya nchi yetu kielimu yameelekea kuweka mbele sana upatikanaji wa cheti ili kupata ajira.

Matokeo yake kama ambavyo tumesoma kwenye vyomba vya habari karibuni vijana wengi wamejikuta wakitafuta vyeti mitaani (fake certificates) kutafutia kazi...hata wengine wanadiriki kutumia vyeti vya namna hiyo kuingia vyuoni. Hiyo ni dhambi ya kipindi hiki na inalingana na dhambi ya kuibia mitihani, nakadhalika. Wanahitimu wetu muendapo kazini muwe wabunifu na siyo watu waliokosa ujasiri wa kuthubutu. Tumewafunza namna ya kupata vitendea kazi hata pale ambapo vitendea kazi vinapokuwa hafifu – remember to improvise.

5 Changamoto
Utoaji wa elimu ya juu unadai maandalizi na uwezo mkubwa katika maeneo mengi. Kwa sasa Tanzania imekuwa na vyuo vingi vya elimu ya juu na hili linaongeza changamoto kwa vyuo vyenyewe. Kati ya changamoto ambazo Chuo Kikuu Ksihiriki cha Mwenge kinakabiliana nazo ni:
    Upatikanaji wa wanafunzi waliofaulu vizuri katika masomo ya kidato cha sita hasa masomo ya sayansi.
    Wanachuo kukosa mikopo ya serikali na hivyo kupangwa chuoni na mwisho wanaamua kurudi nyumbani kwa kukosa uwezo wa kujilipia
    Uendeshaji wa Programu za sayansi ni gharama sana. Hakuna shaka kwamba nchi yetu inahitaji wataalamu wa sayansi na teknolojia ambao watasaidia kusukuma maendeleo ya nchi yetu. Chuo kimeendelea kuwekea mkazo upatikanaji wa wataalamu wa sayansi lakini matumaini yetu kwamba serikali itasaidiana na vyuo vinavyotoa elimu hiyo haujaonekana kupata mwitikio.


    Utoaji wa Scholarships kwa ajili ya wakufunzi wa vyuo vikuu vya binafsi ili wajiendeleze kielimu. Ninachofahamu ni kwamba wanachuo wanapohitimu hapa wanaajiriwa mahali popote na hata serikalini. Tunaomba tupewe nafasi ili wakufunzi wetu waweze nao kusoma zaidi kwa kutumia scholarship za serikali.


Mhashamu Baba Askofu, changamoto ni nyingi lakini kuna ambazo zingeweza kupungua makali kama serikali ingeona vyuo hivi kama washirika wazuri na wenye nia njema ya kutayarisha wataalamu kwa ajili ya Taifa letu na hivyo tupewe ushirikiano wa hali na mali. Ruzuku kwa maeneo kama ya kutayarisha wataalamu wa sayansi ingekuwa uthubutu mkubwa wenye tija kwa upande wa serikali na tunapenda kama Chuo kushauri hivyo.

Mwisho
Mheshimiwa Mgeni Rasmi, napenda kuwaasa wahitimu wetu waende kutimiza wajibu kama Watanzania wazalendo. Mtu ameumbwa na ubinafsi wake lakini wasiuweke ubinafsi mbele bali watende kwa haki wakimtegemea Mungu na kuendelea kusoma. Kusoma hakuna mwisho. Tafadhali wahitimu wetu zingatieni maadili mema na kuendelea kuelimisha wengine bila kumwonea mtu aibu.

Kwa wanachuo mnaobaki tafadhali muendelee kupenda kusoma kwa bidii. Naomba sana msaidiane, mashauriane na kuelekezana ili wote muweze kumaliza masomo yenu vema. Mwenzenu akienda njia isiyo sahihi msisite kumrekebisha kwa upendo na kumsaidia kuelewa wajibu wake wa kusoma na kuishi katika maelekezo na maadili ya mtu mzima mwenye akili na utashi. Mahangaiko na matatizo yatakuwepo lakini kwa njia ya taratibu ya kufuata taratibu za Chuo zilizopo mtafaulu kuzitatua. Pendeni kuwa watu wa kufuata utaratibu na kutumia busara katika kuamua na kuishi maisha yenu.

Mhashamu Baba Askofu, Mkuu wa Chuo, naomba nikushukuru wewe binafsi kwa jitihada unazoweka katika kuchangia kukua kwa elimu nchini. Wengine hapa hawatafahamu lakini naomba kwa ruhusa yako niwaeleze umma huu kwamba wewe na marehemu Askofu Amedeus Msarikie ndiyo mlisimamia kuanzishwa kwa vyuo vikuu vya Kikatoliki Tanzania (vikiwemo Mt. Augustino, Bugando, Ruaha ambacho kiko Jimboni kwako na MWUCE). Aidha shukrani nyingi ziende kwa Mababa Askofu wa Baraza la Maaskofu Katoliki kwa ushupavu na uthubutu wao wa kuwa na vyuo ili kusaidia Taifa la Tanzania likue kimaendeleo. Mchango wa vyuo hivi ni mkubwa sana kwa Taifa Baba Askofu.

Mwisho kabisa nikushukuru tena Baba ASKOFU KWA KUTOLEA MUDA WAKO KUJA KUWATUNUKIA WAHITIMU WETU VYETI VYAO. AHSANTE SANA BABA ASKOFU. KARIBU SANA MWUCE NA JISIKIE NYUMBANI.
Fr. Philbert Vumilia
Mkuu wa Chuo
02-11-2013








All the contents on this site are copyrighted ©.