2013-11-05 11:32:59

Mnaalikwa kwenye Karamu ya Bwana! Wakristo msiridhike kuwa katika orodha ya wageni waalikwa! Mnatakiwa kufanya makubwa zaidi!


Baba Mtakatifu Francisko katika Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, Jumanne, tarehe 5 Novemba 2013 anawaalika waamini kuhakikisha kwamba, wanasherehekea kikamilifu Karamu ya Bwana. Wakristo watambue kwamba, wanaalikwa na Mwenyezi Mungu kushiriki karamu hii wakiwa na dhamiri safi na nyofu.

Karamu ya Bwana ni sherehe inayobubujika furaha, matumaini na mapendo kutoka kwa Kristo; sherehe ambayo inawakumbatia wote pasi na ubaguzi kwani wao ni sehemu ya viungo vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa, kila mtu ana wajibu na dhamana ya kutekeleza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa. Wakristo wajitambue kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya Kanisa la Kristo! Karamu hii ni mwaliko wa kujenga na kudumisha umoja miongoni mwa Wakristo, kila mwamini akijitahidi kujitakatifuza kwa nyenzo mbali mbali zinazotolewa na Mama Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Kanisa linawakumbatia watakatifu na wadhambi; na kwamba, kila mmoja wao ana karama na zawadi ambayo amekirimiwa na Roho Mtakatifu; zawadi ambayo anapaswa kuifanyia kazi barabara kwa ajili ya mafao ya Kanisa. Kanisa linapaswa kuwakumbatia wote kwa kuanzia na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii.

Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Wakristo wamepewa mwaliko na wako kwenye orodha ya waalikwa, lakini bado wanagoma kuhudhuria Sherehe ya Mwanakondoo wa Mungu kwa visingizio kibao! Wanashindwa kutambua kwamba, kuingia ndani ya Kanisa ni mwaliko na neema inayowataka waamini kujenga na kuimarisha Jumuiya ya Kikristo, kila mtu akitumia kikamilifu karama na vipaji vyake kwa ajili ya Kanisa na Jirani zake. Kristo anaendelea kuwaalika waamini kufanya hija inayowapeleka kwenye maisha ya uzima wa milele na kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye kiongozi mkuu wa safari hii ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu anasema, Yesu ni mwingi wa huruma na mapendo, hata kwa wale wanaoonesha shingo ngumu kwa mwaliko wake. Anaendelea kuwasubiri kwa saburi na mapendo makuu. Yesu anawapenda watu ambao ni wanyofu na wa kweli katika maisha yao: kwa maneno na matendo.

Inapendeza ikiwa kama Wakristo wote wataweza kushiriki katika Karamu ya Bwana, ili kuonja furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na wala wakristo wasiridhike kwamba, majina yao yameandikwa kwenye orodha ya waalikwa kwenye Karamu ya Bwana, bali wanatakiwa kushiriki bila kutoa visingizio!







All the contents on this site are copyrighted ©.