2013-11-05 10:41:25

Mauaji yanayofanywa na Boko Haram ni ukatili dhidi ya binadamu!


Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, mauaji ya kinyama yaliyofanywa na Kikundi cha Kigaidi cha Boko Haram ni kwenda kinyume cha ubinadamu. Watu 35 waliokuwa kwenye msafara wa harusi walishambuliwa na kuuwawa mwishoni mwa Juma.

Mashambulizi haya yanaendelea kuongezeka licha ya juhudi za Serikali ya Nigeria kupambana fika na vitendo vya kigaidi nchini humo. Boko Haram wanafanya mashambulizi ya kushtukiza kiasi kwamba, inakuwa vigumu kwa vikosi vya ulinzi na usalama kudhibiti vitendo hivi ambavyo vimeendelea kusababisha majanga kwa wananchi wengi wa Nigeria.

Boko Haram anasema, Askofu mkuu Kaigama ni tishio kwa usalama, amani, utulivu na maendeleo ya wananchi wa Nigeria kwa sasa na kwa siku za usoni. Mwanzoni mashambulizi kama haya yalielekezwa kwa Wakristo, lakini sasa watu wengi wanaendelea kushambuliwa bila huruma.

Serikali inapaswa kutekeleza wajibu wake wa kuhakikisha kwamba, amani na utulivu vinarejea tena nchini Nigeria kwa kuzingatia utawala wa sheria. Kanisa linaungana na wote wanaoomboleza kwa kuondokewa na ndugu, jamaa na jirani zao kutokana na vitendo vya kigaidi. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Nigeria kwamba, iko siku moja, amani na utulivu vitaweza tena kutawala nchini Nigeria.







All the contents on this site are copyrighted ©.